Na mwandishi wetu
Chama cha Wandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa) kimetangaza kurejesha tuzo ya Mwanamichezo Bora wa kila mwezi kwa msimu wa 2023-24.
Katibu Mkuu wa Taswa, Alfred Lucas Mapunda (pichani) ameeleza hayo leo Jumanne baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Taswa kilichoketi Aprili 30, mwaka huu, Dar es Salaam.
Imefafanuliwa kuwa tuzo hiyo itaanza kushindaniwa mwezi Julai, na mshindi wake kupatikana Agosti, mwaka huu ambapo itahusisha wanamichezo wanaocheza Tanzania, Watanzania wanaocheza nje ya nchi na michezo yao ikiwa inatambuliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Mapunda alisema kuwa baada ya tuzo hizo za kila mwezi pia kutakuwa na hafla ya utoaji wa tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Tanzania wa Mwaka ambapo mshindi wa jumla atakuwa miongoni mwa washindi wa mwezi.
Kwa mujibu wa Mapunda ambaye pia aliwahi kuwa ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hafla hiyo pia itatoa zawadi kwa wanamichezo wengine waliofanya vizuri kwa mwaka 2023-24.
“Jukumu la uratibu wa tuzo hiyo ya kila mwezi pamoja na ile ya mwaka litasimamiwa na Kamati ya Tuzo za TASWA, ambayo tayari imeshaundwa na itatangazwa hivi karibuni,” alisema Mapunda.
Miaka ya nyuma Taswa ilikuwa na utaratibu wa kutoa tuzo za kila mwezi ambazo baadaye zilisitishwa na kubaki zile za mwaka ambazo pia nazo zilisitishwa.