Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema tayari wameanza mchakato wa kukisuka upya kikosi chao kwa ajili ya kufanya vizuri na kurudisha ufalme wao kuanzia msimu ujao.
Simba inatarajia kumaliza msimu wa pili mfululizo bila taji lolote, kitendo ambacho kimewakera viongozi wa timu hiyo na sasa wameamua kulitumia dirisha kubwa la usajili kukiboresha maradufu kikosi chao.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa tayari kumekuwa na vikao kati yake na Bodi ya Wakurugenzi pamoja na benchi la ufundi kujadili njia sahihi za kupata wachezaji ambao watakiimarisha kikosi chao na kubeba mataji msimu ujao.
“Jambo la msingi ni kuwa tumechukua kilichotokea kama changamoto na kufanya tathmini ya wapi tumekosea na tunatarajia kufanya maboresho makubwa ya kikosi chetu, tunasubiri ripoti ya benchi la ufundi kujua ni mchezaji gani atakuwa sehemu ya mahitaji kwa msimu ujao na yupi atalazimika kuondoka,” alisema Mangungu.
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa wamepanga kufanya usajili mkubwa wa wachezaji wapya pamoja na mipango ya kambi bora ya kabla ya msimu kuhakikisha wanarejesha utawala wao msimu ujao na hilo linawezekana kutokana na mikakati waliyoianza ya usajili.
Simba itashiriki michuano ya Super Cup mwezi Agosti, mwaka huu na mwenyekiti huyo ameeleza kuwa kipimo cha mafanikio ya msimu ujao wanataka kuyaona kupitia michuano hiyo.