London, England
Nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard ameanza kukata tamaa ya kulibeba taji la Ligi Kuu England (EPL) baada ya timu yake kufungwa mabao 3-0 na Brighton ingawa namba bado hazijawatoa kwenye mbio hizo.
“Mambo yatakuwa magumu kwa sasa, ni lazima tuwe wakweli, hali ni ngumu kukabiliana nayo,” alisema Odegaard.
“Hali haiko vizuri kwa sasa, kwa namna tulivyocheza hasa katika kipindi cha pili, sijui nini kilitokea, niwe tu mkweli, naona kama hakuna matumaini kwa sasa,” alisema Odegaard.
Baada ya matokeo ya mechi hiyo iliyochezwa Jumapili hii, sehemu kubwa ya wachezaji wa Arsenal walionekana katika sura za kukata tamaa, vichwa chini, mshangao na kila hali iliyotoa picha ya huzuni.
Wakati Arsenal ikikata tamaa, matokeo hayo yameamsha ari kwa Brighton ambayo sasa inashika nafasi ya sita kwenye EPL na kuibua matumaini ya kuwamo kwenye ‘top four’ ikiwa imefikisha pointi 58.
Matumaini pekee yaliyobaki kwa Arsenal ni maombi ya kuhakikisha Man City inateleza katika mechi tatu zilizobaki, hapo ndipo matumaini ya timu hiyo yatakapofufuka na hiyo ni kama itashinda mechi zake mbili zilizobaki.
Man City kwa sasa inashika usukani EPL ikiwa na pointi 85 katika mechi 35 wakati Arsenal inashika nafasi ya pili ikiwa imekusanya pointi 81 na imecheza mechi 36.
Matokeo mechi za EPL wikiendi hii…
Brentford 2-0 West Ham United
Everton 0-3 Man City
Arsenal 0-3 Brighton
Leeds United 2-2 Newcastle
Aston Villa 2-1 Tottenham
Chelsea 2-2 Nottingham
Crystal Palace 2-0 Bournemouth
Man United 2-0 Wolves
Southampton 0-2 Fulham