Na mwandishi wetu
Ruvu Shooting imekuwa timu ya kwanza kuaga Ligi Kuu NBC baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka Simba mtanange uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi , Dar es Salaam.
Timu hiyo imeteremka baada kushuka uwanjani mara 28 na kukusanya pointi 20 baada kushinda michezo mitano, sare tano na kufungwa mara 18.
Kocha wa Ruvu Shooting, Mbwana Makata alisema kuwa kipigo hicho ni rasmi kimewashusha Ligi Kuu NBC lakini kushuka kwao kumechangiwa na mambo mengi kubwa ni kukosa wachezaji wenye ubora kikosini mwake.
“Wachezaji hawakuwa na ubora, kwenye usajili hatukuwa na fungu, tulimpata mchezaji mmoja Valentino Mashaka. Kama leo ubora wa wachezaji wa Simba umeamua matokeo lakini ukiangalia mipango yetu kama benchi la ufundi ilikuwa inaonekana.
“Tumeshuka lakini changamoto hazikimbiwi, unajifunza kitu, nimejifunza nini cha kufanya, wakati mwingine kama mwalimu natakiwa kufanya kazi ili ninapopata timu nyingine nijue nini cha kufanya,” alisema Makata.
Naye Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema kuwa amefurahishwa na kiwango walichoonyesha wachezaji wake kwenye mchezo huo na sasa anaangalia michezo miwili iliyosalia.
“Nimefurahia ushindi wa leo kwa sababu mbili, kwanza tumecheza vizuri halafu pia tumepata mabao mengi, hilo ndilo kubwa,” alisema Robrtinho raia wa Brazil.
Alisema kuwa ni jambo jema kucheza soka safi na kupata ushindi mnono sababu inaongeza furaha kwa mashabiki ambao wamekuwa sehemu ya familia yake ndio maana alikuwa akishangilia pamoja nao kwenye mabao yaliyokuwa yakifungwa.
Hivi karibuni, ofisa habari wa klabu hiyo, Masau Bwire (pichani juu) ambaye amejijengea umaarufu kwa kutoa kauli za kuwatisha wapinzani wake kabla ya mechi, alinukuliwa na GreenSports akizungumzia ugumu wa timu hiyo kucheza Ligi Kuu NBC msimu ujao.