Na mwandishi wetu
Kamati ya Maadili ya TFF imewafungia maisha kutojihusisha na soka Mwenyekiti wa Kitayosce, Yusuph Kitumbo na kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe kwa kosa la upangaji matokeo.
Wawili hao wanadaiwa kujihusisha na upangaji matokeo katika mechi ya Ligi ya Championship kati ya Fountain Gate FC na Kitayosce iliyochezwa Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Gairo, Morogoro.
Taarifa iliyowekwa leo Ijumaa na TFF kwenye kursa zake za mitandao ya kijamii ilisema kamati hiyo katika kikao chake kilichofanyika Mei 11, mwaka huu imewatia hatiani kwa kuzingatia Ibara ya 73(9) (b) ya kanuni za Maadili za TFF, toleo la mwaka 2021.
Taarifa hiyo ilieleza, Kitumbo hakufika mbele ya kamati hiyo bila kutoa udhuru wowote wa maandishi ya kupokea wito wakati Mwakingwe aliwasilisha utetezi wake kwa njia ya maandishi.
Hii ni mara ya pili Kitumbo kufungiwa maisha kujihusisha na soka kwa upangaji matokeo kwani Aprili 4, 2016 alikutwa na hatia hiyo pia.
Baada ya kuitumikia adhabu hiyo kwa mwaka mmoja mnamo Julai 20, 2017 Kitumbo aliachiwa huru na kuendelea na shughuli za soka.
Soka Mwakingwe, Kitumbo wafungiwa maisha
Mwakingwe, Kitumbo wafungiwa maisha
Read also