Na mwandishi wetu
Yanga imetanguliza mguu mmoja katika kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya jioni ya leo Jumatano kuifumua Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa mabao 2-0.
Wanajangwani hao walifanikiwa kuandika ushindi huo katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali kupitia kwa mabao ya Stephanie Aziz Ki na Bernard Morrison.
Mtanange huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ulianza kwa timu zote kuonesha kuheshimiana huku Yanga ikipoteza nafasi nyingi za kupata mabao ya uongozi.
Mfano Fiston Mayele alishindwa kuitumia nafasi ya wazi dakika ya 25 baada ya kupiga shuti jepesi lililookotwa na mlinda mlango Washington Arubi aliyeonesha kiwango kizuri kwenye mechi hiyo.
Dakika tatu baadaye Mayele alipata nafasi nyingine akiwa anawahadaa vizuri mabeki wawili waliokuwa wakimkaba lakini akapiga shuti lililopaa juu ya lango la wapinzani wao.
Dakika 45 za kwanza zilitamatika bila ya nyavu za timu yoyote kutikisika kabla ya Marumo waliokuwa ‘wamepooza’ eneo la ushambuliaji kufunga dakika ya 33 kupitia kwa Katlego Otladisa lakini mwamuzi alionesha kuwa mfungaji aliotea.
Marumo walianza kipindi cha pili kwa kasi ambapo dakika ya 49 Otladisa alipiga shuti ndani ya 18 lakini mpira ukapita kidogo nje ya lango la Yanga.
Dakika ya 55 Ranga Chivaviro wa Marumo alikosa bao baada ya kumhadaa vizuri beki wa Yanga, Ibrahim Bacca lakini shuti lake lilipita nje kidogo ya lango. Hiyo ni baada ya kupokea pasi ya mwisho ya kisigino kutoka kwa Ismael Toure.
Marumo waliendelea kulisakama lango la Yanga huku wakiutawala mchezo na kupiga udambwidambwi wa ‘shibobo’ mpaka dakika ya 64 Yanga walipofanya shambulio la kushtukiza kupitia kwa Tuisila Kisinda.
Akitokea pembeni ya uwanja, Kisinda alimfinya beki kabla ya kutoa pasi ya chini kwa Aziz Ki aliyemchambua Arubi ndani ya 18 kwa shuti kali na kumuacha akiwa hana la kufanya.
Yanga ikaanza kutakata upya na kuonekana kutamba zaidi eneo la katikati ya uwanja hasa baada ya kuingia kwa Mudathir Yahya na Salum Aboubakar ‘Sureboy’ waliochukua nafasi za Aziz Ki na Yanick Bangala kwenye dakika ya 65 ya mchezo.
Ilibaki kidogo Mayele afunge bao lake la sita kwenye michuano hiyo msimu huu lakini mpira alioupiga kwa kuunyanyua akimhadaa kipa uligonga mwamba wa juu na kuokolewa na mabeki. Mayele alifanya hivyo akipokea pasi murua ya juu iliyopigwa na Mudathir dakika ya 83.
Morrison aliyeingia dakika ya 65 kuchukua nafasi ya Jesus Moloko alihitimisha karamu ya Yanga kwa kufunga bao dakika ya 90.
Kabla ya kufunga Morrison ambaye alipewa pasi na Mayele na kubaki na kipa, alitaka kumpiga chenga Arubi kwa kuupiga mpira juu yake lakini wakagongana na mfungaji akadondoka kabla ya kunyanyuka na kuuwahi mpira huo alioupiga na kujaa nyanvuni.
Kwa ushindi huo Yanga sasa inasubiri hatma ya mechi ya marudiano itakayopigwa Mei 17, mwaka huu Uwanja wa Royal Bafokeng, Rustenburg kuanzia saa 1.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, ikihitaji sare ya aina yoyote au kutopoteza kwa zaidi ya bao 1-0 ili kutinga fainali.
Marumo yenyewe inaendelea kuwa na wiki ya huzuni kutokana na kupokea kipigo kama hicho kutoka kwa Mamelodi Sundowns siku nne zilizopita katika mechi ya Ligi Kuu Afrika Kusini ambako inapambana isishuke daraja ikiwa katika nafasi ya 14 kati ya timu 16.
Kimataifa Yanga yatanguliza mguu fainali Shirikisho
Yanga yatanguliza mguu fainali Shirikisho
Read also