Madrid, Hispania
Bao la Kevin de Bruyne limeiwezesha Man City kutoka sare ya ugenini ya bao 1-1 mbele ya Real Madrid katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Matokeo hayo yaliyopatikana jana Jumanne yanakuwa mwanzo mzuri kwa City ambao watajipanga kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani Jumatano ijayo ili kupata ushindi katika mechi ya marudiano na kufuzu hatua ya fainali kwa mara ya pili.
Iwapo azma hiyo ya City itafanikiwa, timu hiyo itakuwa na kibarua cha mwisho katika fainali kwa kuumana na timu mojawapo mahasimu wa Italia kati ya Inter au AC Milan ambazo zitaanza kuisaka tiketi hiyo leo Jumatano.
City pia itakuwa imejiweka vizuri katika mbio za kubeba mataji matatu msimu huu ikiwa vizuri kwenye mbio za kulibeba taji la Ligi Kuu England na Juni 3 itaumana na Man United katika mechi ya fainali ya Kombe la FA
Man City iliutawala vyema mchezo kipindi cha kwanza lakini kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois alikuwa makini na kuwanyima Rodri, Erling Haaland na De Bruyne nafasi za kuipatia City mabao.
Zikiwa zimebakia dakika 10 timu kwenda mapumziko, Vinicius Jr aliwageuzia kibao City na kuwapa raha mashabiki wa Real Madrid kwa bao alililofunga kwa shuti la umbali wa mita 25.
Dakika ya 67, De Bruyne naye alimaliza kazi kwa kufunga bao la kusawazisha na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa City waliosafiri hadi Madrid.
Nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya leo, Jumatano, Mei 10…
AC Milan v Inter Milan
Kimataifa De Bruyne aibeba City ugenini
De Bruyne aibeba City ugenini
Read also