Na Hassan Kingu
Raha ya kususa upate mtu sahihi wa kumsusia, kususa au kutingisha kiberiti vyote hivyo vinategemea na unayemsusia au kumtingishia kiberiti, akikubaliana na wewe umeula, akikataa umeumia.
Ndicho ninachokiona kwa kiungo wa Yanga na timu ya Taifa, Feisal Salum au Fei Toto, ni bahati mbaya sana mabosi wa Yanga wamekataa kususiwa, wamekataa kutingishiwa kiberiti na mchezaji huyo.
Matokeo yake mtingisha kiberiti au msusaji ameshindwa kupata alichotaka, matarajio yake yamekwama na hadi sasa hatujui hatma yake.
TFF, imeendelea kuyatupa maombi ya mchezaji huyo kupitia wanasheria wake kutaka uamuzi wa awali wa kumrudisha Yanga ufanyiwe mapitio ili aruhusiwe kuvunja mkataba na klabu ya Yanga.
Matokeo ya TFF ni kama yamemuacha njia panda mchezaji huyo, hataki kukubaliana na kamati, anataka Yanga wamuache aondoke, Yanga nao hawataki na hata wakitaka masharti yatakuwa balaa.
Fei Toto si mchezaji wa kwanza kutingisha kiberiti au kususa kwa nia ya kutaka kuhama ili kusaka changamoto mpya au kutafuta maslahi makubwa zaidi.
Tunaambiwa mbinu hiyo imekuwa ikitumiwa sana na Benard Morisson, ingia toka zake katika Yanga na Simba amezifanikisha kwa staili hiyo hiyo, na tunaambiwa tusishangae tukisikia tena amerudi Simba kwa staili hiyo hiyo ya kutingisha kiberiti na kupaisha thamani yake.
Emmanuel Okwi, mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga na baadaye Simba naye inadaiwa alikuwa makini na mahiri katika kutingisha kiberiti na ndio maana haikushangaza akacheza Simba, akaenda Yanga, akarudi Simba na zipo habari kwamba Simba walimchoka na hawakumruhusu tena awatingishie kiberiti.
Pengine kosa ambalo naliona kwa Fei Toto ni namna alivyosusa au alivyitingisha kiberiti, si kama kina Okwi na Morisson (pichani chini) ambao inaonekana walikuwa makini au mabosi wa Simba na Yanga walizama katika mtego wa wachezaji hao na kukubaliana nao.

Kwa Fei Toto katika hali ya kawaida ingetegemewa aombe kuongezewa mkataba na hapo hapo maslahi yake yaboreshwe lakini hili la kuvunja mkataba ni gumu kwa sababu linahitaji ridhaa ya pande mbili na inadaiwa kwamba upande mmoja ulihofu kwamba alikuwa akielekea kwa mahasimu wao.
Ni jambo la kawaida mfanyakazi/mchezaji kutaka maslahi zaidi hasa pale anapoona kazi anayoifanya ni kubwa na anacholipwa hakiendani na ukubwa wa kazi yake na hapo hapo kuna ambao hawafanyi anachokifanya yeye lakini mshahara wao ni mkubwa mara mbili au tatu kumzidi.
Hata hivyo mambo haya ya kutafuta maslahi makubwa yana taratibu zake hasa inapotokea watumishi/wachezaji wakiwa wamefungwa na mikataba, ni lazima anayetaka haki ya nyongeza ya ujira aangalie mkataba na kutafuta namna ya kudai maslahi hayo bila ya kukiuka masharti ya mkataba.
Kwa Fei Toto habari zinadai kwamba naye alitaka alipwe kama kina Mayele, Moloko, Tuisila, Morisson na wengineo hasa akizingatia kazi ambayo amekuwa akiifanya ni kubwa na nzuri kuwazidi hao wenzake na wengineo ambao wanasugua benchi lakini katika ujira wamemuacha mbali.
Kama nilivyosema awali katika kuidai haki hiyo kuna mkataba, kabla ya kuamua unatingisha vipi kiberiti, angalia kwanza mkataba wako kama unakupa nafasi ya kufanya hivyo.
Na ndio maana si sahihi hata kidogo kujilinganisha na mtumishi/mchezaji mwenzako kwani kila mmoja kaingia na mkataba wake na makubaliano yake, jiangalie wewe na mkataba wako.
Ulikuwa mfanyakazi/mchezaji wa JKU au Singida Big Stars ukapata kazi Yanga, makubaliano yako ya kuingia Yanga au mkataba wako hauwezi kuwa sawa na mwenzako aliyekuwa akifanya kazi TP Mazembe. Tukubaliane hapo kwanza.
Kwa hiyo kama wewe uliingia Yanga kwa ujira wa Sh400,000 usione ajabu mwenzako kutoka TP Mazembe akaingia kwenye ajira hiyo hiyo kwa ujira wa Sh1,500,000.
Mwenzako kaajiriwa kwa hadhi ya timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho Afrika na wewe umeajiriwa kwa hadhi ya timu ya Ligi Kuu NBC au Ligi Kuu Zanzibar.
Wewe mshahara wako ulikuwa Sh 200,000 umekwenda Yanga ukapewa nyongeza hadi Sh 400,000, mwenzako alikuwa pengine akilipwa Sh 2,000,000 pengine kaja Yanga wakampunguzia hadi Sh 1,500,000 au wakamuongezea hadi Sh 2,500,000.
Sasa ikitokea mwenzako kiwango chake kimeshuka, hana msaada kwenye timu hilo si kosa lake wala si kosa lako, huwezi kumtumia yeye kama mfano katika kusaka maslahi yako, yeye ana mkataba wake na wewe una mkataba wako, utumie mkataba wako kusaka maslahi yako.
Huo ndio uhalisia wa ulimwengu wa kisasa hasa katika soka, hata hao tunaowasikia huko Ulaya kila mtu anaingia na mkataba wake, ikitokea mwenye mchango mkubwa kwenye timu ana mshahara mdogo hawezi kumtumia mwenye mshahara mkubwa kudai haki zake, atapigania yeye mwenyewe kwa kuangalia mkataba wake.
Ni ama ataongezewa mkataba au ataangalia taratibu za kuuvunja na si kujiaminisha kwamba unaweza kuvunja mkataba kwa kurudisha pesa kwenye akaunti ya bosi wako, ni lazima mkae mezani muangalie namna ya kukubaliana kuuvunja mkataba.
Ukiona yote hayo magumu angalia namna nzuri ya kususa ambayo itakusaidia ama uvunjiwe mkataba, uuzwe au uruhusiwe kuondoka au maslahi yako yaboreshwe.
Zipo habari kwamba kuna baadhi ya wachezaji wanapotaka kupigania maslahi wana namna ‘nzuri’ ya kususa ikiwamo kutengeneza majeraha feki, kuomba ruhusa za mara kwa mara kwa visingizio vya wagonjwa, misiba na mengineyo.
Mwisho wa siku ni yule unayemsusia au kutimtingishia kiberiti kama atakasirika na kuamua kuvunja mkataba wako utakuwa umepata ulichokitaka, vinginevyo akiamua tofauti, mchezaji au mtumishi unaweza kujikuta pagumu kama ilivyo kwa Fei Toto.
Hivi karibuni kuna hoja imetambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa hakuna mkataba usiovunjwa, ni kweli lakini tatizo unauvunjaje, hapa kwa mtazamo wangu ndipo alipokosea Fei Toto.