Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema kikosi chake kipo kamili, kina ari na watacheza kwa tahadhari mechi ya kesho Jumatano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Nabi amezungumza hayo leo Jumanne jijini Dar es Salaam akisema pia wanaingia kwenye mechi hiyo wakifahamu ubora wa Marumo mpaka wanafika nusu fainali bila ya kutazama hali mbaya waliyonayo kwenye Ligi ya Afrika Kusini.
Alisema kuelekea mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.00 jioni, amewasoma wapinzani wao hivyo wanaingia na tahadhari zote katika mtanange huo.
“Wachezaji wote wana utimamu wa mechi ya kesho, maandalizi yamekwenda kama tulivyopanga, wachezaji wamejiandaa kikamilifu, tumeisoma timu pinzani, wachezaji wako tayari kupambana na wana ari ya kucheza na Marumo.
“Niwapongeze Marumo ni timu nzuri japo kwenye ligi yao hawafanyi vizuri lakini kwenye michuano hii wanafanya vizuri, kila mechi wamepata bao na wameitoa Pyramids, hivyo hiyo si timu ya kubeza, tutacheza kwa umakini mkubwa kulingana na wapinzani tunaokutana nao ukizingatia ni mechi za mikondo miwili, nyumbani na ugenini,” alisema Nabi.
Nabi raia wa Tunisia pia aliwashukuru mashabiki wa Yanga kwa ushirikiano waliowapa mpaka sasa, akiwataka kuongeza nguvu hiyo kesho kwa kushangilia na kuwapa nguvu wachezaji hata inapotokea Yanga haina mpira kwa wakati huo.
Naye Raymond Mdaka, kocha msadizi wa Marumo alisema hawawezi kuzungumzia maandalizi yao kwa undani kwa sababu ni sehemu yao ya kazi ya kila siku kutokana na mechi za michuano hiyo na za ligi walizonazo kila wakati ingawa wamewasoma Yanga kuelekea mechi hiyo.
“Tumekuwa tukifanya maandalizi kila baada ya mechi moja kuelekea nyingine, tunachojua timu zina utofauti na huwezi kubadili kucheza kila mechi iliyo mbele lakini kuna vitu tumeangalia kama ugumu wao, namna wanavyocheza hivyo hakukuwa na maandalizi makubwa japo tupo tayari kwa kila mchezo ulio mbele yetu,” alisema Mdaka.
Timu hizo zinashuka dimbani zikiwa na uwiano tofauti kwenye ligi zao ambapo Yanga ni kinara wa Ligi Kuu NBC kwa pointi 71 wakati Marumo ipo nafasi ya 14 kwa pointi 29.
Marumo ambayo imeifunga Pyramids ya Misri jumla ya mabao 2-1 kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho, kwenye michezo yao mitano ya mwisho ya ligi wameshinda mmoja, wakidroo mitatu na kufungwa mmoja.
Yanga wao ambao wamefungwa mechi moja kwenye mechi tano za ligi zilizopita na kushinda nne, iliiondosha Rivers United ya Nigeria kwa jumla ya mabao 2-0 na kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza kama ilivyo Marumo.