Na mwandishi wetu
Timu ya Azam imeeleza kuwa kuna mengi yamewakwamisha msimu huu wasifanye vizuri kwenye Ligi Kuu NBC lakini wamefurahi mno kutinga fainali ya Kombe la FA (ASFC).
Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ (pichani) amesema matarajio yao yalikuwa mengine kwenye ligi lakini ilipofikia sasa hawana cha kubadili zaidi ya kujipanga kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye fainali ya Kombe la FA.
Jumapili iliyopita, Azam iliifunga Simba mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Nangwanda, Mtwara na sasa inasubiri mshindi wa mechi ya Singida BS dhidi ya Yanga icheze naye fainali.
Akitaja miongoni mwa sababu zilizowakwamisha kufanya vizuri kwenye ligi na kushindwa kuwania ubingwa licha ya kufanya usajili mzuri, Popat alisema ni kukandamizwa kwenye baadhi ya maamuzi ya mechi za ligi, kukosa matokeo ugenini huku akieleza wamejipanga kuhakikisha wanayamaliza hayo msimu ujao.
“Imeonekana tumesajili vizuri lakini bado tumekwama, kwa hiyo unaweza kupata jibu pamoja na kusajili vizuri lakini bado si suluhisho, Mungu amejaalia mechi imeisha tumeshinda 2-1 lakini tumenyimwa penalti ya wazi kabisa.
“Miaka mingine iliyopita tushafungwa kwenye mstari, mpira unarudishwa ndani tunafungwa, msimu huu pia tumefungwa na mkubwa mwingine mpira unatoka, unarudi ndani unafungwa, hatuna namna nyingine ya kubadilisha hali hiyo.
“Timu za Kariakoo ni kubwa kuliko sisi ndiyo maana tukiwafunga furaha yetu inakuwa kubwa sana, lakini pia timu nyingine tunazokutana nazo wao wanajipanga zaidi kwa kufahamu ni wadogo na sisi ni wakubwa kwa hiyo unakuta zinatusumbua kwenye matokeo,” alisema Popat.
Mtendaji huyo alisema safari hii wamefanya vizuri zaidi kwenye mechi za nyumbani kuliko ugenini hivyo hiyo pia ni sababu inayowaangusha ingawa tayari benchi la ufundi limeanza kulifanyia kazi hilo ili kubadili mwenendo msimu ujao na kufanya vizuri zaidi.
Kwenye ligi Azam inashika nafasi ya tatu kwa pointi 53 ikifuatiwa na Singida BS yenye pointi 51. Yanga SC iko kileleni kwa pointi 71, Simba ni ya pili ikiwa na pointi 64 baada ya timu zote kucheza mechi 27 zikisalia mechi tatu kufungwa rasmi pazia la ligi kuu msimu wa 2022-23.