Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama amesema kwenye mechi waliyofungwa jana Ijumaa na Wydad kwa penalti 4-3, walifanya kila walichokijua ili wapate ushindi lakini mwisho wamekubali matokeo.
Simba ilitolewa na Wydad katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika jana kwenye Uwanja wa Mohamed V, Casablanca baada ya matokeo ya jumla ya bao 1-1 ambapo kila timu ilishinda bao 1-0 kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Chama aliandika ujumbe huo leo Jumamosi kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na kueleza kuwa matokeo hayo wanayachukulia kama chachu ya kuzidi kuimarika zaidi kimapambano.
“Imekuwa safari ndefu yenye mambo mengi ndani yake na hisia mchanganyiko. Jana tulifanya kila kitu tunachokijua lakini mwisho wa siku ilibidi tukubaliane na ukweli ili tuweze kusonga mbele,” alisema.
“Tutachukulia matokeo ya jana kama chachu ya kuendelea kuimarika zaidi. Asanteni kwa ushauri na jumbe zenu za kututia moyo. Mungu awabariki sana,” aliandika Chama aliyefunga mabao manne kwenye michuano hiyo.
Mchezaji huyo pia alikosa penalti yake aliwashukuru kwa dhati wachezaji wenzake, benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, mwekezaji wao, Mohammed Dewji na mashabiki wa Wekundu hao akifafanua maombi na upendo wao ndio umewafikisha walipo sasa.
Timu hiyo pia imeripotiwa kuanza safari yake leo Jumamosi mchana ya kutoka jijini Casablanca nchini Morocco kurejea Tanzania kuendelea na ratiba za michuano mingine inayowakabili.
Katika safari hiyo, timu hiyo ilitarajia kupitia Doha, Qatar kabla ya kikosi hicho kutua jijini Dar es Salaam asubuhi ya kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Katika misimu mitano iliyopita Simba imeishia robo fainali mara nne. Ilitolewa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwenye Ligi ya Mabingwa wakati msimu uliopita kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ilitolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti 4-3.