London, England
Kipa wa Tottenham Hotspur, Hugo Lloris ametaka mashabiki wa timu hiyo waombwe radhi baada ya kufungwa mabao 6-1 na Newcastle, matokeo ambayo pia yameathiri mbio zao katika top four kwenye Ligi Kuu England.
Spurs ingeweza kufungana pointi na Newcastle kama ingepata ushindi badala yake ilijikuta ikibugizwa mabao matano katika dakika 21 za kwanza na mwishowe kulala kwa mabao 6-1 ugenini St James Park.
Sehemu kubwa ya mashabiki wa Tottenham waliosafiri hadi St James Park kwa ajili ya mechi hiyo iliyochezwa jana Jumapili walianza kutoka uwanjani kabla ya muda wa mapumziko.
“Inakatisha tamaa tunalazimika kuwaomba radhi mashabiki, hatukuonyesha kitu kizuri na hatukuweza kulingana kiwango na wachezaji wa Newcastle,” alisema Lloris ambaye alifanyiwa mabadiliko wakati wa mapumziko.
“Tulikuwa nyuma katika kila uneo la kiuchezaji na tulikosa sehemu muhimu ya mwanzo ya mchezo, kipindi cha pili habari ilikuwa tofauti kabisa lakini ni jambo linaloumiza,” alisema.
“Si suala la mbinu, hatukujaribu japo kupambana na tulichelewa kwa kila kitu, kwa sasa ni vigumu japo kuangalia kiwango chetu cha uchezaji,” aliongeza.
Kwa matokeo hayo Spurs inabaki katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 53 baada ya mechi 32 lakini wamezidiwa pointi sita na Newcastle inayoshika nafasi ya tatu huku ikiwa na mechi moja pungufu jambo ambalo linafifisha matumaini ya timu hiyo kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
“Unaweza kupigwa mara moja au mbili lakini sisi ilikuwa kama vile hatukuwa wenye kupambana, Newcastle wanatakiwa kupewa sifa zao kwa kuuanza mchezo wakiwa vizuri, walijua nini hasa cha kufanya,” alisema Lloris ambaye pia ni nahodha wa Spurs.
Matokeo ya mechi za EPL wikiendi hii…
Bournemouth 0-4 West Ham
Newcastle 6-1 Tottenham
Fulham 2-1 Leeds United
Brentford 1-1 Aston Villa
Crystal Palace 0-0 Everton
Leicester 2-1 Wolverhampton
Liverpool 3-2 Nottingham Forest