Barcelona, Hispania
Kocha wa Barca, Xavi Hernandez amesema winga wake nyota mwenye miaka 15, Lamine Yamal (pichani) hana woga na amemjumuisha kwenye kikosi kitakachocheza na Atletico Madrid leo Jumapili.
Yamal ambaye ni zao la akademi ya La Masia inayomilikiwa na Barca, Julai mwaka huu atafikisha miaka 16, anatarajiwa kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuichezea timu kubwa ya Barca katika mechi rasmi.
“Ni mchezaji ambaye anaweza kutusaidia kwa sababu ana kipaji,” alisema Xavi akimzungumzia Yamal ambaye ana asili ya Morocco.
“Ana mambo mengi binafsi, ana kipaji, anaweza kuutumia vizuri mpira wa mwisho, anaongoza wachezaji, ana nguvu, tunamzungumzia mchezaji ambaye anaweza kuweka alama katika zama fulani kwenye klabu,” alisema Xavi.
Yamal, ambaye baba yake ana asili ya Morocco na mama yake anatokea Equatorial Guinea, alizaliwa Julai 13 mwaka 2007 na amekuwa kwenye kikosi cha akademi ya Barca tangu akiwa na miaka mitano.
Kama atacheza mechi ya leo dhidi ya Atletico, Yamal ataweka rekodi ya kucheza mechi hiyo rasmi akiwa na miaka 15 na siku 285.
Kwa sasa rekodi ya mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza mechi rasmi katika klabu hiyo inashikiliwa na Armand Martinez Sagi ambaye alicheza mechi dhidi ya Real Gijon Aprili 2, 1922 akiwa na miaka 15, miezi 11 na siku tano.
Xavi ambaye pia ni zao la akademi ya Barca alisema kwamba ni vigumu kumlinganisha Yamal na wachezaji wengine.
“Ana kipaji cha pekee, ni kizazi kipya, tofauti iliyopo na zama zangu ni kwamba kwa sasa hawana uwoga, Yamal yuko tofauti, ana vitu vya wachezaji mbalimbali, sijaona ulingano wa moja kwa moja na yeyote,” aliongeza Xavi.
Barca inashika usukani La Liga kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya Real Madrid iliyo nafasi ya pili ingawa hivi karibuni imekuwa na matokeo yasiyo ya kuridhidhisha ya mechi mbili mfululizo dhidi ya
Getafe na Girona zilizoisha kwa sare ya bila kufungana.