Na mwandishi wetu
Bakari Nondo Mwamnyeto leo Jumapili amekuwa ‘mpishi’ mzuri wa pasi za mabao yaliyofungwa na Fiston Mayele na kuifanya Yanga itoke na ushindi wa 2-0 mbele ya Rivers United ya Nigeria katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mayele alifunga bao la kwanza dakika ya 73 baada ya Mwamnyeto kuunasa mpira karibu kidogo na eneo la kati, akamchungulia Mayele na kumuunganishia pasi na Mayele kuukokota kidogo mpira kabla ya kuujaza wavuni.
Dakika saba baadaye Yanga waliandika bao la pili, safari hii bao hilo lilitokana na mpira wa adhabu uliopigwa langoni mwa Yanga baada ya Khalid Aucho kumchezea rafu mchezaji mmoja wa Rivers.
Moloko aliunasa mpira huo wa adhabu na kuambaa nao kwa kasi kabla ya kumsogezea Mwamnyeto ambaye kwa mara nyingine alimchungulia Mayele na kumuunganishia pasi ambayo Mayele hakufanya ajizi kuujaza mpira wavuni.
Mayele alianza kulichachafya lango la Rivers katika dakika ya 65 baada ya Aziz Ki kuchomoka na mpira upande wa kulia na kumpunguza beki mmoja kabla ya kutoa pasi ya kimo cha mbuzi ambayo Mayele aliiunganisha vizuri kwa kichwa lakini hakuweza kuipatia Yanga bao.
Baada ya mabao ya leo Mayele sasa anafikisha mabao matano katika michuano ya Kombe la Shirikisho msimu huku akifikisha mabao 12 kama utachanganya na mabao aliyofunga wakati Yanga ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kuangukia Shirikisho.
Ushindi huo wa ugenini katika mechi ya kwanza ya robo fainali, Yanga imeupata takriban saa 24 baada ya mahasimu wao Simba nao kupata ushindi wa nyumbani wa bao 1-0 kwa Wydad Casablanca katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga hata hivyo ina kila sababu za kijivunia ushindi wao kwa kuwa umepatikana ugenini na ni mtaji mkubwa kabla ya timu hizo kurudiana takriban wiki moja ijayo katika mechi ambayo Yanga itakuwa mwenyeji na matokeo yake yataamua timu ipi itacheza hatua ya nusu fainali.
Katika hatua ya nusu fainali Yanga iwapo itafuzu itakutana na mshindi wa mechi nyingine ya robo fainali kati ya Marumo Gallant ya Afrika Kusini na Pyramids ya Misri.
Ushindi wa leo pia ni kama imelipa kisasi kwani imewahi kutolewa na Rivers katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa jumla ya mabao 2-0, ikifungwa nyumbani bao 1-0 na ugenini ikikutana na kipigo kama hicho.
Kimataifa Mayele aizamisha Rivers Nigeria
Mayele aizamisha Rivers Nigeria
Read also