Na mwandishi wetu
Msafara wa wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga umetuasalama nchini Nigeria Ijumaa hii na kupata mapokezi mazuri kutoka kwa wenyeji wao, Rivers United.
Yanga iliondoka nchini Alhamisi alfajiri kupitia Addis Ababa na kutua Lagos kisha kuanza safari ya kuelekea Mji wa Uyo ambako ndiko utakapofanyika mchezo huo Jumapili hii.
Akizungumza kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya Yanga, meneja wa timu hiyo, Walter Harison ameeleza kuwa hali za wachezaji wao tangu wawasili Nigeria zipo sawa na wana ari kubwa kuelekea mchezo huo.

“Nashukuru tumefika salama hapa Uyo na wenyeji wetu wametupokea vizuri kifupi kwamba jeshi letu lipo katika hali nzuri, hali ya hewa ni rafiki kabisa na kwa mujibu wa ratiba ya kocha tukiwa hapa tutafanya mazoezi mara mbili kabla ya siku ya mchezo,” alisema Walter.
Meneja huyo ameeleza kuwa wakiwa Lagos, kocha wao mkuu Nasreddine Nabi alizungumza na wachezaji na kuwataka wasiwadharau wapinzani wao zaidi wanapaswa kuongeza umakini na kufanya kila jambo kwa usahihi ili kupata matokea mazuri.
Alisema katika mchezo huo, wamejipanga kuhakikisha wanaandika historia mpya kwa timu hiyo kutinga nusu fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika na anaamini hilo litawezekana kutokana na ubora na maandalizi mazuri waliyoyafanya.

Ili kufikia malengo na kuweka historia kwa kufika robo fainali Yanga inalazimika kushinda mchezo huo ili kujitengenezea mazingira rahisi kwenye mchezo wa marudiano ambao utachezwa Aprili 30, mwaka huu Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.