Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema anaujua ubora wa Wydad AC kuelekea mechi yao ya Jumamosi hii lakini anaamini wana nafasi ya kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo.
Robertinho ameyaeleza hayo kuelekea mchezo wao huo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.
Alisema anafurahi kutimia kwa siku za kucheza mechi hiyo na kwamba kwenye Ligi ya Mabingwa hakuna mchezo mwepesi na wapinzani wao wana uwezo, mipango na ni timu bora lakini anaamini wamejipanga vya kutosha na wana nafasi ya kushinda.
“Nina furaha tunacheza kesho, hakuna mchezo mwepesi kwenye Ligi ya Mabingwa, Wydad wana uwezo, mipango na timu bora, lakini sasa ni nafasi nzuri kwa Simba kwa sababu kwangu ni wakati mzuri ndani ya uwanja.
“Kwangu soka ni sanaa na sera yangu ni kucheza na kupata matokeo mazuri, tuna kiwango kizuri kwangu ni muhimu sana kushinda mchezo wa nyumbani,” alisema Robertinho.
Kuhusu Simba kufungwa nyumbani na ugenini kwenye hatua ya makundi dhidi ya Raja Casablanca ambao nao wanatoka Morocco, Robertinho alisema wamefanyia marekebisho makosa yaliyowafanya kupoteza na ameweka umakini ili kupata ushindi katika mchezo huo.
“Tupo tayari kwa mchezo na ninaamini tutashinda, sababu wachezaji wangu wana ari kubwa ya kupambana. Najua utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora waliokuwa nao wapinzani wetu lakini tupo tayari kwa mapambano lengo ni kupata ushindi,” alisema.
Simba itamkosa kipa wake Aishi Manula kutokana na majeraha aliyoyapata kwenye mchezo wa Kombe la FA (ASFC) dhidi ya Ihefu na siku ya Jumatatu atapelekwa kuonana na madaktari bingwa ili aangaliwe kama anahitaji kufanyiwa matibabu zaidi.
“Kwa sasa hatuwezi kusema atakuwa nje kwa msimu mzima lakini niseme anahitaji kufanyiwa matibabu makubwa ili aweze kurejea kwenye milingoti mitatu,” alisema Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally.
Viingilio vya mchezo huo kwa mzunguko ni Sh 5,000, viti vya rangi ya machungwa 10,000, VIP C Sh 15,000 VIP B Sh 20,000 na VIP A Sh 30,000. Tiketi za Platinum Sh 150,000 ambazo watapata usafiri maalum wa kwenda na kurudi uwanjani na wakiwa uwanjani watapata chakula na kinywaji bure.
Kimataifa Robertinho: Naujua ubora wa Wydad
Robertinho: Naujua ubora wa Wydad
Read also