Na mwandishi wetu
Beki wa kushoto wa Ihefu, Yahya Mbegu ameeleza juu ya kuwaniwa na timu za Simba SC na Singida Big Stars, akifafanua kinachomkwamisha mpaka sasa kufanya maamuzi ni maslahi yake binafsi.
Mbegu anayesifika kwa ubora wake amekuwa akitajwa kuwaniwa na timu hizo huku ikielezwa kuwa tayari ameshamalizana na Singida iliyo chini ya Hans Pluijm lakini ameieleza GreenSports kuwa bado hajamwaga wino kokote.
“Bado sijasaini kokote ila kuhusu kuhitajika na timu ni kweli, ni timu nyingi zimekuja za ligi kuu na bado sijamalizana na yoyote, kuna timu nimefika nazo kwenye maongezi tu lakini bado hatujakubaliana,” alisema.
“Ishu kubwa ni maslahi yangu binafsi kama mchezaji, hapa Ihefu mkataba wangu unaenda mwisho na hata wao pia nimezungumza nao na kukubaliana nao kwa asilimia 80 ila bado tunazungumza,” alisema Mbegu.
Mchezaji huyo aliyewahi kuitumikia timu ya vijana ya Simba amekiri kuwa anapenda changamoto mpya lakini anahitaji kufikiria zaidi kabla ya kufanya maamuzi kuhusu mustakabali wake bila ya kuangalia ukubwa wa timu inayomuhitaji.
Mbegu aliyewahi kukipigia Mwadui na Polisi Tanzania, ametua Ihefu kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea Geita Gold alikocheza kwa nusu msimu.