Munich, Ujerumani
Sadio Mane amerejea kikosini Bayern Munich tayari kuivaa Man City katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku kocha Thomas Tuchel akitarajia maajabu ili kupindua matokeo baada ya kulala kwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza.
Mane alisimamishwa akidaiwa kumpiga ngumi mchezaji mwenzake, Leroy Sane katika mechi ya kwanza na leo Jumatano watakuwa wenyeji wa Man City katika dimba la Alianza Arena mjini Munich wakisaka tiketi ya nusu fainali.
Tuchel alisema kwamba zinahitajika jitihada za kipekee kutoka kwa kila mtu anayehusika na klabu ya Bayern ili kujizuia kutolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya tatu.
“Tunahitaji kufanya maajabu, kwa hakika yatakuwa maajabu,” alisema Tuchel kocha wa zamani wa Chelsea aliyekabidhiwa jukumu la kuinoa Bayern Machi 25 mwaka huu baada ya Nagelsmann Julian kutimuliwa.
“Ni kazi ngumu na utakuwa mlima mkubwa kuupanda, tunahitaji kuamini, kujiamini sisi wenyewe lakini hatutaki kuwa watu wa kuota, kuota kwangu ni karibu kabisa na kulala, kama hatutaweza kufanya lolote basi pia hatutakiwi kulala japo kwa sekunde moja.” alifafanua Tuchel.
“Tunatakiwa kuamini na kuyafanya mambo yawezekane kutokana na kiwango chetu cha uchezaji, ari na nguvu, tupo sisi na timu yetu, tuna wachezaji wenzetu, mashabiki ambao wapo tayari kupigana pamoja nasi na baada ya hapo tunatakiwa kuwa wakweli katika hali halisi,” alisema Tuchel.
“Kama utaangalia kileleni kwenye mlima hapo utajiwa na hisia kwamba una mzigo umekuelemea kwa hiyo tutafanya hatua kwa hatua, nusu kwa nusu na changamoto ni ngumu mno, tunatakiwa kuwa na ujasiri na kuangalia ukubwa wa mlima, tutaianza safari na kuwa tayari kuendelea nayo hadi mwisho,” alisema.
Kuhusu Mane ambaye alikuwa akitumikia adhabu ya faini na kukosa mechi moja na tayari aliikosa mechi na Hoffenheim iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, Tuchel alisema klabu imeshafikia hitimisho katika suala la mchezaji huyo na atacheza mechi ya Jumatano (leo).
“Sadio yupo kikosini, hatuzungumzii tena mkasa ule, uamuzi ulishachukuliwa, tunatakiwa kusubiri siku ya mechi ili kuona kama ataanza kwenye kikosi cha kwanza au ataanzia benchi,” alisema Tuchel.
Katika mechi zilizochezwa jana Jumanne, Chelsea ililala kwa mabao 2-0 mbele ya Real Madrid na hivyo kuziaga rasmi fainali hizo kwa kufungwa jumla ya mabao 4-0 baada ya kipigo kama hicho katika mechi ya kwanza.
Nayo AC Milan ilifuzu nusu fainali baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Napoli na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza.
Mechi za leo Jumatano robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya
Bayern Munich v Man City
Inter Milan v Benfica
Matokeo mechi za jana Jumanne za robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya
Chelsea 0-2 Real Madrid
Napoli 1-1 AC Milan