Na mwandishi wetu
Kipigo cha mabao 2-0 ambacho Yanga ilikipata Jumapili iliyopita dhidi ya Simba kimemuibua nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto akiwataka wachezaji na mashabiki wa timu hiyo kusahau yaliyopita.
Mwamnyeto badala yake amewataka wote kuelekeza akili zao kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United.
Yanga ilipokea kichapo cha mabao 2-0, kutoka kwa watani zao katika mchezo wa Ligi Kuu NBC uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, matokeo ambayo yameonesha kupunguza ari ya baadhi ya wachezaji na mashabiki wa timu hiyo.
Mwamnyeto amesema kuwa wanapaswa kusahau yaliyopita na kuweka nguvu kwenye mchezo unaowakabili ili kushinda na kuandika historia kwa kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.
“Kufungwa ni sehemu ya mchezo ingawa kufungwa na mtani inauma lakini tunapaswa kukubaliana na uhalisia, imeshatokea na sasa ni vyema tukahamisha fikra zetu kwenye mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Rivers United ambao unahitaji utimamu wa akili na mwili,” alisema Mwamnyeto.
Beki huyo alisema kuhusu kipigo cha Simba anamini uwezo wa kulipiza kisasi wanao endapo watakutana nao kwa mara nyingine kwenye mashindano ya Kombe la FA (ASFC) lakini kwa sasa ni vyema wakasahau yaliyopita.
Alisema maumivu ya kufungwa na Simba hayalingani na yale ya kutolewa kwenye hatua ya robo fainali na Rivers United hivyo ni bora wakaweka pembeni matokeo ya mchezo dhidi ya watani zao na kuwawaza zaidi wapinzani wao wa Caf.
Yanga Jumapili ijayo itakuwa ugenini Nigeria ikiumana na Rivers United huo ukiwa mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa Dar es Saalam Aprili 30, mwaka huu.