Na mwandishi wetu
Baada ya mapumziko ya siku moja kikosi cha Yanga leo Jumanne kimerejea mazoezini kujiwinda dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Imeelezwa kuwa kikosi hicho kinajifua vikali, ikielezwa kuwa kinajiandaa kuwafuata wapinzani wao hao keshokutwa Alhamisi kwa ajili ya mechi hiyo ya mkondo wa kwanza.
Yanga inaingia kwenye kibarua hicho baada ya Jumapili iliyopita kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu NBC.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kikosi hicho kimeanza mazoezi kikiwa na tafakari juu ya mchezo unaokuja wakitaka kurekebisha makosa ya mchezo uliopita wakiwa na ari ya kutafuta matokeo ugenini.
“Kulingana na ratiba ilivyo, tutaondoka kuelekea Nigeria kwa ajili ya maandalizi ya mwisho tukiwa kule dhidi ya Rivers, matokeo yaliyopita hata wachezaji wanafahamu hayakuwa mazuri kulingana na ukubwa wa mchezo wenyewe na wanajiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi ijayo tupate matokeo mazuri,” alisema Kamwe.
Yanga itakipiga na Rivers Jumapili hii majira ya saa 10 jioni kwa saaa za Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa Taifa wa Godswill Akpabio, Akwa Ibom.
Timu hiyo inayonolewa na Nasreddine Nabi inaivaa Rivers ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa na kufurushwa kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita kwa kufungwa na timu hiyo bao 1-0 katika michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.
Soka Yanga yaanza kujifua Dar
Yanga yaanza kujifua Dar
Read also