Manchester England
Klabu ya Manchester City nayo imeingia katika mbio za kuisaka saini ya kiungo wa Borussia Dortmund na timu ya Taifa ya England, Jude Bellingham ambaye pia anawaniwa na Real Madrid.
Bellingham ambaye ndio kwanza ana miaka 19 ametokea kuwa tishio ndani ya kikosi cha Dortmund na sasa anasakwa na klabu kadhaa Ulaya ingawa Man City na Real Madrid ndizo zinazotajwa zaidi.
Wakati ikidaiwa kwamba Real Madrid tayari ilishatuma wawakilishi wake nchini Ujerumani kwa ajili ya mazungumzo ya kumsajili Bellingham, Man City kwa sasa wanachofanya ni kupata uhakika kama mchezaji huyo atakuwa tayari kufanya kazi na kocha Pep Guardiola.
Awali ilielezwa kwamba Real Madrid walimtengea kitita cha Pauni 88 milioni na wako tayari kupanda dau wakati Man City wao wanachotaka kwanza ni uhakika kama yuko tayari kufanya kazi na Pep.
Haijaweza kueleweka mara moja iwapo, Real Madrid bado wana nia ya kumsajili mshambuliaji wa Man City Erling Haaland na kama mchezaji huyo ataungana na Bellingham Real Madrid au nguvu ya klabu hiyo sasa imehamia kwa Bellingham.
Zimewahi kuwapo habari kwamba katika mkataba wa Haaland na Man City kuna kipengele kinachompa nafasi ya kujiunga na Real Madrid lakini Pep amewahi kukanusha kuwapo kwa kipengele hicho katika mkataba wao na Haaland.
Kama ilivyo kwa Bellingham, Haaland naye kabla ya kutua Man City mwanzoni mwa msimu huu, hapo kabla alikuwa akiichezea Dortmund.
Kimataifa Man City nayo yamtaka Bellingham
Man City nayo yamtaka Bellingham
Read also