Manchester, England
Kipa wa zamani wa Man United, Peter Schmeichel (pichani juu) amewalaumu wachezaji wa timu hiyo ‘kwa kushindwa kujiongeza’ baada ya mchezaji mwenzao Lisandro Martinez kuumia na kubebwa na wachezaji wa timu pinzani.
Kuumia kwa mchezaji huyo kulitokea jana Alhamizi katika mechi ya Europa Ligi kati ya Sevilla na Man United iliyopigwa kwenye dimba la Old Trafford na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Katika mechi hiyo Man United ilijikuta katika wakati mgumu baada ya kufungwa mabao mawili ya kusawazisha katika dakika 10 za mwisho huku wachezaji wake Martinez na Raphael Varane wakiumia.
Kuumia kwa Martinez ndiko kulikomuibua Schmeichel kipa aliyetwaa taji la Ligi Kuu England mara tano akiwa na Man United ambaye alisema hakuvutiwa na namna wachezaji wa Man United walivyoruhusu mchezaji huyo kusaidiwa kutolewa uwanjani na wachezaji wa Sevilla.

“Ilionekana kama wachezaji wa Sevilla walikuwa watu wazuri kwa kumbeba na kumtoa uwanjani. Hapana, walitaka atoke ili mambo yao yaende vizuri,” alisema Schmeichel akizungumza na BBC.
“Kwa kumbeba hawakupunguza kasi yao, Man United walishatumia wachezaji wao watano wa akiba na kwa hiyo walifahamu asingeweza kurudi uwanjani,” alisema Schmeichel.
“Tukio lile halikumpa kocha au wachezaji wasaa wa kufanya mazungumzo, wachezaji wa United walitakiwa kuzuia jambo lile, ilitakiwa aachwe uwanjani, waachwe madaktari wamfuate na kumbeba wao na kumtoa nje na katika kipindi hicho mnajipanga upya,” alisema.
“Hili ni jambo ambalo wachezaji wanahitaji kulifanya, kilichotokea ni kutojiongoza uwanjani, Harry Maguire alitakiwa kusimamia jambo hilo, kocha anapoona mchezaji wake anabebwa na wachezaji wawili wa timu pinzani anatakiwa kuzuia jambo hilo,” aliongeza Schmeichel.