Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Pluijm amesema kuwa wapo kwenye mikakati mizito ya kuivua Yanga ubingwa wa Kombe la FA (ASFC).
Singida itacheza na Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Liti, Singida hivi karibuni.
Pluijm ameeleza kuwa anajua ubora waliokuwa nao wapinzani wao lakini amepanga kuutumia mchezo wa ‘derby’ dhidi ya Simba ili kujua namna ya kuwakabili wapinzani wao.
“Lazima nikiri Yanga ni timu bora kwa sasa Tanzania unapokutana nayo lazima uwe na mbinu zaidi ya moja ili kupata unachokitaka ndio maana pamoja na mikakati tuliyokuwa nayo lakini mchezo wao wa derby dhidi ya Simba utatuongezea mbinu za kuwakabili,” alisema Pluijm.
Kocha huyo aliyewahi kuinoa Yanga, alisema anajua haitokuwa kazi rahisi kutokana na uwezo waliokuwa nao wachezaji wa timu hiyo lakini watawabana kuhakikisha wanatimiza malengo yao hasa ukizingatia mchezo huo utachezwa kwao Singida.
Pluijm amewataka wachezaji wake kutumia mchezo huo kuthibitisha ubora waliokuwa nao na kupigania malengo ya timu ili msimu ujao iweze kuliwakilisha taifa kwenye michuano ya klabu Afrika.