Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Geita Gold, Elias Maguli amekiri timu yao kushindwa kutimiza lengo lao msimu huu na sasa wanajipanga kumaliza mechi zao nne zilizobaki kwa ushindi ili kutetea nafasi yao.
Geita iliyojinasibu kuwa itamaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC, mpaka sasa inashikilia nafasi ya tano ikiwa haiwezi kuzifikia pointi za Azam inayoshikilia nafasi ya nne, hata kama itashinda michezo yote iliyosalia.
Azam inashikilia nafasi ya nne ikiwa imekusanya pointi 50, Geita ikifuatia kwa pointi zake 37 hesabu ambazo zinaitoa timu hiyo katika nafasi ya nne.
“Kwa sasa tunagombania kumaliza hapahapa kwenye nafasi ya tano na tunawania nafasi hiyo na Namungo ambao tumewazidi pointi mbili tu, mechi zinazokuja ni ngumu zaidi sababu tutacheza na timu ambazo ziko chini zinataka kujinasua.
“Kila mchezo uliobaki ni fainali kwetu ili kuhakikisha tunamaliza nafasi ya tano maana nafasi ya nne ni ngumu sasa hivi hivyo tunataka kumaliza hapa kwenye tano na tunashukuru mno mashabiki kwa sapoti yao mpaka sasa wasituache mpaka mwisho,” alisema Maguli.
Geita imebakisha michezo miwili nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City kisha itakuwa ugenini kukamilisha mechi zake za ugenini dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar.