Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya KMC FC, umemfuta kazi aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Thiery Hitimana na mikoba yake kupewa Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Taarifa ya kufutwa kazi kwa kocha huyo raia wa Rwanda imetolewa leo Alhamisi baada ya kikao cha uongozi wa timu kufanyika asubuhi na kufikia uamuzi wa kumuondoa Hitimana na benchi lake kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo kwenye Ligi Kuu NBC.
Mwenyekiti wa Bodi ya KMC, Songoro Mnyonge ameeleza kuwa malengo ya timu yao tangu kuanzishwa kwake ni kupigania ubingwa lakini kwa msimu huu imekuwa tofauti ndio sababu wakaamua kuchukua maamuzi hayo.
“Haya ni maamuzi ya bodi yote ya KMC, na hatukufanya peke yetu, tumemshirikiana na kocha Hitimana mwenyewe na waliokuwa wasaidizi wake na kukubaliana, kifupi tunawatakia kila la heri huko waendako,” alisema Mnyonge.
Kiongozi huyo pia alisema wamempa kazi Julio hadi mwisho wa msimu huu kutokana na uwezo wake na wanaamini atairudisha timu hiyo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi katika mechi nne zilizosalia.
Akiwa hapo Julio amepewa nafasi ya kupendekeza watu wa kufanya naye kazi, lengo likiwa ni kuondoa mgongano wa mawazo katika kukisuka kikosi chao ili kiweze kufanya vizuri kwenye michuano wanayoshiriki kwa sasa.
KMC inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi ikiwa na alama 26, ambapo katika michezo mitano ya mwisho ya ligi imeshinda mchezo mmoja pekee na kufungwa minne.