Na mwandishi wetu
Simba imeitambia Ihefu FC baada ya kuichapa mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Highland Estate, uwanja ambao mahasimu wao Yanga waliumia kwa kupigwa mabao 2-1.
Ihefu ambayo iliichafua Yanga kwenye uwanja huo kwa kuizuia kuweka rekodi ya kufikisha mechi 50 bila kupoteza hata moja, ilitarajiwa ingeibana Simba kama mahasimu wao Yanga lakini haikuwezekana.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumatatu hii, Simba ilineemeka kwa mabao ya mshambuliaji wake mahiri Jean Baleke ambaye sasa anafikisha mabao saba ya ligi na kufikisha mabao 14 katika mashindano yote.
Baleke pia ndiye aliyeifunga Ihefu mabao matatu peke yake katika ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya timu hiyo katika mechi ya Kombe la Shirikisho Azam (FA) iliyopigwa Alhamisi iliyopita jijini Dar es Salaam.
Ikicheza bila mastaa wake wa kikosi cha kwanza wakiwamo Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Aishi Manula na wengineo, ilipata mabao yake katika dakika 10 za mwisho, la kwanza likifungwa dakika ya 83 na la pili dakika ya 87.
Kwa ushindi huo Simba sasa inafikisha pointi 60 ikiwa imezidiwa pointi tano na Yanga lakini imecheza mechi 25 wakati Yanga imecheza mechi 24 na Jumanne itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar.
Baada ya mechi na Kagera, Yanga itaumana na mahasimu wake Simba Aprili 16 katika mechi ambayo Yanga itapenda kushinda ili kuimarisha matumaini yake ya kulitetea taji la ligi hiyo wakati Simba itataka ushindi ili kupunguza pengo la pointi na kuweka sawa matumaini ya kulibeba taji hilo.
Soka Simba yatamba ilipoumia Yanga
Simba yatamba ilipoumia Yanga
Read also