Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amewapongeza wachezaji wake akisema walistahili ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ihefu jana Jumatatu kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbeya.
Mgunda alisema amefurahi kuona timu hiyo imepata matokeo hata baada ya kubadili kikosi katika mechi hiyo na kuanzisha wachezaji wengi ambao hawapati nafasi katika michezo iliyopita msimu huu.
“Unajua siku zote ukiwa mwalimu lazima uwe na moyo wa kuthubutu, wote waliocheza wamesajiliwa, wanapaswa kuitumikia Simba, ni lini watapata nafasi ni jambo jingine na ikifika wakati wao unawapa na unawaeleza wanapaswa kuonesha kwanini wamesajiliwa Simba.
“Nashukuru kuona wamefanya kazi nzuri, wamejituma hawajacheza muda na maelekezo tuliyowapa kama benchi wameyafanyia kazi, wamejituma tunamshukuru Mungu, tunajipanga na mechi ijayo,” alisema Mgunda.
Akizungumzia mabadiliko ya dakika 21 ya kumtoa Ismael Sawadogo na kuingia Nassor Kapama, Mgunda alisema ni mabadiliko ya kawaida na kwamba inawezekana imeshtua wengi lakini lilikuwa ni suala la kiufundi ambalo lilileta matunda mwishowe.
“Mabadiliko hayana muda wala haijalishi ni nani, ilikuwa mabadiliko ya kuongeza ufanisi uwanjani na mwisho yameleta matunda. Kumtoa mchezaji haimaanishi ni mbovu, inawezekana siku hiyo hayuko sawa au haendani na maelekezo ya wakati huo,” alisema Mgunda.
Naye Kocha Msaidizi wa Ihefu, Zuberi Katwila aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza wakifuata mipango waliyopanga ingawa alifafanua maamuzi ya mwamuzi kidogo yalivuruga mchezo na kusababisha wapoteze umakini lakini makosa yao madogo pia yalichangia.
“Si kazi yetu kumhukumu mwamuzi lakini si benchi letu wala la Simba tulikuwa tunamshangaa mwamuzi, amepoa anashindwa kwenda na mchezo, nashindwa kuelewa ni nini, yote kwa yote wachezaji wamefanya vizuri, kuna makosa madogo yametokea na huwezi kulaumu beki ni makosa ya kimpira yanatokea bila kukusudia,” alisema Katwila.
Simba imepata ushindi huo wa pili mfululizo dhidi ya Ihefu ndani ya siku nne baada ya awali kuifunga mabao 5-1 kwenye robo fainali ya Kombe la FA iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.