Na mwandishi wetu
Ripoti ya matibabu ya wachezaji wa Simba, kipa Aishi Manula (pichani) na beki Henock Inonga imeondoa hofu kuhusu kuumia kwa wachezaji hao ikieleza kuwa wanaendelea vizuri, watajiunga na wenzao mazoezini.
Wachezaji hao walishindwa kumaliza dakika 90 katika mechi ya robo fainali Kombe la FA (ASFC) dhidi ya Ihefu ambapo Simba ilishinda kwa mabao 5-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Daktari mkuu wa Simba, Edwin Kagoba alisema kuwa wachezaji hao waliumia lakini baada ya kuwapeleka hospitali na kuwafanyia vipimo wamebaini maumivu waliyopata ni ya kawaida.
“Siku ya pili baada ya mchezo tuliwapeleka Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya vipimo zaidi na majibu yalipotoka juzi, yamebaini wana maumivu ya kawaida, tumewapa mapumziko ya siku tatu, timu itakaporudi kutoka Mbeya wataungana na wenzao kuendelea na mazoezi,” alisema Kagoba.
Taarifa hiyo imerudisha furaha na tabasamu kwa benchi la ufundi pamoja na mashabiki wa timu hiyo hasa ukizingatia mchango wa wachezaji hao kwenye kikosi cha Simba na ugumu wa mashindano yanayowakabili kwa sasa.
Simba ipo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imepangwa kucheza dhidi ya mabingwa watetezi Wydad Casablanca.
Kwenye Ligi Kuu NBC inaendelea kupambana, ipo nafasi ya pili ikipambana kurudisha taji hilo ambalo walilibeba kwa misimu minne mfulululizo kabla ya msimu uliopita kuporwa na mahasimu wao Yanga.
Simba pia wapo hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA wakitarajia kuumana na Azam FC ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye robo fainali iliyopigwa Azam Complex.