Milan, Italia
Klabu ya Juventus imepewa adhabu kwa mashabiki wake kutoruhusiwa uwanjani katika mechi ya Kombe la Italia baada ya kumtolea maneno ya ubaguzi wa rangi mshambuliaji wa Inter Milan, Romelu Lukaku.
Katika adhabu hiyo sehemu ya Uwanja wa Allianz, jukwaa la kusini, mashabiki hawataruhusiwa kutumia jukwaa hilo, adhabu ambayo itaanza msimu ujao katika mechi ya kwanza ya Juve ya Kombe la Italia.
Lukaku alikutana na kadhia hiyo Jumanne iliyopita katika mechi ya nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Italia iliyoisha kwa sare ya 1-1 huku bao la kusawazisha la Inter likifungwa na Lukaku katika dakika tano za nyongeza.
Kadhia za kibaguzi dhidi ya Lukaku ilitokea baada ya mshambuliaji huyo kufunga bao la Inter kwa mkwaju wa penalti na kuwaonyesha mashabiki wa Juve ishara ya kuwataka wakae kimya.
Lukaku aliweka vidole vyake mdomoni kama vile kuwaambia ‘fungeni midomo yenu’ kitendo ambacho kilionekana kuwakera mashabiki hao waliojibu mapigo kwa kumtolea kauli na ishara za ubaguzi wa rangi.
Kwa kosa la kuwaonyesha mashabiki ishara ya kuwataka wafunge midomo yao, Lukaku alipewa kadi ya
pili ya njano na hivyo naye ataikosa nusu fainali ya pili ya michuano hiyo ambayo itapigwa Aprili 26.
Ishara hiyo ya Lukaku pia inadaiwa kuwatia hasira baadhi ya wachezaji na kusababisha mzozo ambapo katika tukio hilo winga wa Juve, Juan Cuadrado na kipa wa Inter, Samir Handnovic nao walipewa kadi nyekundu kila mmoja pamoja na faini ya dola 11,000 pia kwa kila mmoja.
Katika siku za hivi karibuni matukio ya ubaguzi wa rangi yameripotiwa nchini Ujerumani na Hispania kwa wachezaji kukutana na kadhia hiyo wakati wakiziwakilisha timu zao.
Beki wa RB Leipzig, Benjamin Henrichs alilalamikia kupokea kauli za kibaguzi kupitia Instagram baada ya timu yake kuichapa Borrusia Dortmund mabao 2-0 katika mechi ya Kombe la Ujerumani.
Jumanne iliyopita mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Jr alitoa ushahidi mbele ya vyombo vya sheria dhidi ya shabiki wa Mallorca aliyemtolea maneno ya kibaguzi katika mechi ya La Liga ambapo mchezaji huyo amesema kwamba hatokubali kuombwa msamaha.
Kimataifa Lukaku aiponza Juventus
Lukaku aiponza Juventus
Read also