Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Pluijm amesema hayupo tayari kuzungumza lolote kuhusu timu hiyo kumuwania kipa wa Simba, Beno Kakolanya kwa sasa.
Pluijm amezungumza hayo baada ya hivi karibuni kuwepo kwa taarifa za Singida kumuwania kipa huyo ambaye hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Wekundu hao huku mkataba wake ukielekea ukingoni.
Duru mbalimbali za michezo zimeeleza kuwa tayari viongozi wa Singida wameshazungumza na kipa huyo wa zamani wa Prisons na mambo yameshakaa sawa lakini Simba ikionesha kutokubali kumwachia kipa huyo.
Pluijm amekiri kuwa anahitaji wachezaji wapya wenye ushindani mkubwa kama watafanikiwa kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini amekiri kuwa hiki si kipindi cha kuweka wazi mipango hiyo.
“Hapana kwa sasa siwezi kuzungumzia majina yanayohusishwa na sisi, wakati wake bado lakini lengo kubwa ni kupata wachezaji wenye ushindani mkubwa endapo tutafanikiwa kushiriki michuano ya Afrika msimu ujao, tukifika hapo tutazungumza lolote,” alisema Pluijm.
Singida inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu inapambana kumaliza kwenye nafasi hiyo ili ikate tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Timu hiyo pia ipo hatua ya robo fainali ya Kombe la FA, ikipambana kutwaa kombe hilo ili iwakilishe taifa katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.