Na mwandishi wetu
Baada ya Yanga kutua salama Lubumbashi, DR Congo, kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi amewataka wachezaji wake kusahau matokeo yaliyopita na kuelekeza akili na mawazo yao kwenye mchezo wa Jumapili hii.
Yanga ipo Libumbashi kukamilisha mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe.
Yanga tayari imeshafuzu hatua ya robo fainali lakini inahitaji ushindi katika mchezo huo ili imalize kileleni kwenye msimamo wa Kundi D na kuweka heshima kwa kuifunga Mazembe mechi zote mbili.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Yanga iliifunga Mazembe mabao 3-1.
Yanga inaongoza kundi hilo kwa pointi 10 sawa na US Monastir inayoshika nafasi ya pili lakini Wanajwangani hao wapo kileleni kutokana na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Real Bamako ya Mali inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano huku Mazembe ikiburuza mkia pia ikiwa na pointi tatu.
Nabi ameeleza kuwa pamoja na wenyeji wao Mazembe kutokuwa na nafasi ya kusonga mbele lakini wanahitaji kupata ushindi ili kumaliza kwa heshima mechi za hatua ya makundi.
“Tunapaswa kuthibitisha ubora wetu kwa kushinda ugenini mbele ya TP Mazembe, ili hilo lifanikiwe lazima kusahau matokeo yaliyopita na kutowadharau wapinzani kwa mwenendo mbovu waliokuwa nao lazima kila mmoja wetu awajibike ili tufikie malengo kwenye mchezo huu,” alisema Nabi.
Kocha huyo ameeleza kuwa mapokezi mazuri waliyoyapata Lubumbashi kutoka kwa wenyeji wao pamoja na kundi kubwa la mashabiki kuonekana kuwaunga mkono havitoshi kuwapa pointi tatu.
Nabi badala yake anasema kwamba kitu cha msingi ni kucheza kwa kupambana muda wote wa mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mazembe saa 10 jioni.
Nabi ameeleza kuwa amezungumza na wachezaji wake kuhusu hilo baada ya mazoezi ya kwanza leo Ijumaa asubuhi na imani yake ni kwamba wamemuelewa na watatimiza kile ambacho uongozi wa Yanga umewaagiza.
Katika mchezo huo, Yanga inatarajiwa kukosa huduma ya kipa wake namba moja Djigui Diarra na kiungo Khalid Aucho kila mmoja akiwa na kadi mbili za njano walizopata kwenye mechi zilizopita.