London, England
Nahodha na mshambuliaji wa timu ya Taifa ya England, Harry Kane amesema anataka kuweka rekodi ya kuifungia timu hiyo mabao 100 jambo ambalo amekiri ni gumu lakini si kwamba haliwezekani.
Kane ambaye pia anaichezea Tottenham Hotspur, Jumapili iliyopita alifikisha mabao 55 na timu hiyo alipofunga bao katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Ukraine katika mechi ya kuwania kufuzu Euro 2024.
Kwa sasa Kane ndiye kinara wa mabao wa wakati wote wa England akiwa amempiku nyota wa zamani wa timu hiyo, Wayne Rooney aliyekuwa akishikilia rekodi hiyo akiwa amefunga mabao 53.
“Kwa hakika kufunga mabao 100 litakuwa jambo gumu lakini mimi siwezi kuliondoa kabisa, bado kijana nina miaka 29, bado niko fiti na imara na nataka niichezee England kadri nitakavyoweza,” alisema Kane.
“Kila mechi nitakuwa najiweka tayari kwa ajili ya kucheza, tutakwenda hatua kwa hatua, kwa sasa hatua inayofuata ni kufikisha mabao 60,” aliongeza Kane.
“Siwezi kufuta suala la kufunga mabao 100, litakuwa jambo gumu hasa lakini tunatakiwa kuona miaka michache ijayo itakwendaje,” alisema Kane.
England itaumana na Malta na North Macedonia Juni mwaka huu katika mechi nyingine ya kuwania kufuzu Euro 2024.
Rooney aliifungia England mabao 53 katika mechi 120 kuanzia mwaka 2003 hadi 2018 alipostaafu rasmi kuichezea timu hiyo wakati Kane ameanza kuichezea England mwaka 2015 na hadi sasa ameichezea mechi 82.
Kinara mwingine wa mabao wa England ni Bobby Charlton ambaye anashika nafasi ya tatu akiwa ameifungia timu hiyo mabao 49 katika mechi 106 kuanzia mwaka 1958 hadi mwaka 1970.