Na mwandishi wetu
Makocha na wachezaji wa zamani wamewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaitendea haki ahadi ya Sh milioni 500 iliyotolewa na Serikali endapo watafuzu michuano ya Mataifa Afrika (Afcon).
Wakongwe hao wakizungumza na GreenSports leo Jumanne, pia walitoa pongezi kwa hamasa hiyo wakiamini itasaidia kama ilivyokuwa kwenye klabu nchini zinazoshiriki michuano ya klabu Afrika.
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Bakari Malima alisema: “Naona Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) ameingia na mguu mzuri, timu zote zinaonesha kitu kwa kufanya vizuri na hii hamasa naamini itakwenda kutusaidia kwenye mbio hizi za Afcon, cha msingi vijana watambue umuhimu wa hamasa hii.
“Lakini pia nashauri sasa angehamia na huku chini ili kutengeneza vyema vijana ambao huko watakuwa wanapambana zaidi bila ya hamasa kwa kuanza kuwekeza sasa huku chini.”
Beki wa zamani wa Simba, Amri Said alisema hamasa hiyo itasaidia kuzipa ari saikolojia za wachezaji kuelekea kwenye mechi hizo na inatoa ishara kwamba nchi nzima iko nyuma ya Stars kwa kuwa Serikali yenyewe ndiyo imetoa ahadi hiyo na Wananchi wako nyuma.
“Kwa kifupi, hii maana yake ni kwamba Mama anawaambia vijana sisi tupo nyuma yenu, tunawajali hivyo kila mchezaji afahamu kinachoendelea sasa ingawa mchezo ni mgumu kila tunapokutana na Uganda lakini naamini kwa nguvu iliyowekwa na benchi la ufundi lililopo tutafanya vizuri,” alisema Said.
Aliyewahi kuwa kocha wa Stars, Charles Mkwasa (pichani juu) alisema kwake hajawahi kuona hamasa ya namna hiyo nchini, akiwataka wachezaji na makocha kuwa makini na kuwekea mkazo ahadi hiyo kwa kufikia lengo husika.
Alisema anafahamu mtihani uliopo mbele ya Stars ni mgumu lakini pia akawataka wafahamu hata kiasi cha milioni 500 si kidogo hivyo wapambane na kutilia maanani kauli kama hiyo ya Serikali kwa faida ya taifa zima.
Winga wa zamani wa Simba na Yanga, Edibily Lunyamila alisema: “Rais wetu ameonesha njia, ametoa hamasa Simba na Yanga, zimefanyiwa kazi, sasa amegeukia Stars ni nzuri sababu wachezaji inawaongezea kitu na ukizingatia wengi wametoka Simba na Yanga hivyo wanafahamu utamu wa ahadi hizi, wazifanyie kazi kweli.
“Japo niseme kwamba mechi yetu ya kwanza na Uganda sio nyepesi, wako vizuri mara nyingi tunapokutana nao lakini safari hii nadhani mseto uliopo Stars utatusaidia kupata matokeo.”
Motisha hiyo imetangazwa juzi na Waziri wa Utamaduni, Sana na Michezo, Pindi Chana kuelekea mchakato wa Stars kufuzu Afcon wakianza na mechi mbili dhidi ya Uganda zitakazochezwa Machi 24 na 28, mwaka huu.
Tayari Stars imetua nchini Misri kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kwanza unaotarajia kupigwa mjini Alexandria kabla ya mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.