Na mwandishi wetu
Timu ya Ihefu imeeleza kuwa inajipanga vilivyo kuhakikisha inavaana na Simba kwenye mechi mbili mfululizo za michuano tofauti na kuibukia kidedea dhidi ya Wekundu hao.
Ihefu ambayo ilikuwa na mapumziko ya siku tano, imerejea mazoezini jana kuanza rasmi mawindo yao hayo ya mechi ya robo fainali ya Kombe la FA na ile ya ligi, zote dhidi ya Simba zinazotarajiwa kupigwa Aprili, mwaka huu.
Kocha Msaidizi wa Ihefu, Zuberi Katwila ameiambia GreenSports kuwa wanafahamu kibarua hicho dhidi ya Wekundu hao na kwa kuwa ni mechi mbili zenye hadhi tofauti basi wanafahamu tofauti ya namna ya kujipanga nazo ili zote wapate matokeo.
“Tuko kwenye kujiandaa dhidi ya Simba, ni mechi mbili tofauti, hivyo maandalizi ya Kombe la FA yatakuwa ni ya dakika 90 na ligi yatakuwa namna ya kutafuta pointi, yaani tunajipanga kwa namna mechi husika inavyotaka na lengo ni kupata ushindi mechi zote.
“Lengo letu ni kuvuka kwanza hapa tulipo kwa maana ya kusonga nusu fainali ya Kombe la FA, tutakayekutana naye mbele naye tutajua namna ya kufanya, ni hatua moja baada ya nyingine na tunajipanga kwa ajili ya kufanya vizuri,” alisema Katwila.
Licha ya kuteka hisia za wengi kwa timu hizo kukutana mara mbili mfululizo kwenye michuano tofauti lakini pia kiwango ilichonacho Ihefu hivi karibuni kimekuwa gumzo zaidi.
Ihefu ambayo ilianza vibaya ligi, imeshinda mechi nne na sare moja katika mechi zake tano zilizopita huku pia ikisifika kuwaadhibu vigogo kila wanapokuwa uwanja wao wa nyumbani.
Iliichapa Azam bao 1-0 kwenye mechi ya mwisho na ndiyo timu pekee iliyoifunga Yanga msimu huu kwa ushindi wa mabao 2-1.