Madrid, Hispania
Klabu ya Real Madrid imewageuzia kibao mahasimu wake Barcelona katika tuhuma za kutoa rushwa kwa mwamuzi ikiahidi kutoa ushirikiano kwenye vyombo husika.
Inadaiwa kwamba uamuzi huo umefikiwa baada ya Rais wa Real Madrid, Florentino Perez kuitisha ‘kikao cha dharura’ kwa ajili ya kujadili tuhuma za rushwa zinazoikabili klabu ya Barcelona au Barca.
Hoja za Real Madrid zimekuja baada ya waendesha mashitaka kudai kwamba Barca walimlipa Euro milioni 8.4 mwamuzi Jose Maria Negreira kupitia kampuni yake, malipo ambayo sasa yanatiliwa shaka na kuhisiwa kuwa ni hongo.
Negreira ambaye ni makamu rais wa kamati ya waamuzi ya Hispania, anadaiwa kupokea fedha hizo kati ya mwaka 2001 na 2018 ingawa mabosi wa Barca wamekana kutoa malipo hayo kwa nia ya kuhonga.
Badala yake Barca wamedai malipo hayo yametolewa kwa kampuni ya Negreira kwa ajili ya ushauri wa kiufundi ambapo fedha hizo pamoja na mambo mengine zilitolewa ili kukusanya video za kuwasaidia maofisa wa benchi la ufundi la klabu hiyo.
Negreira pamoja na marais wa zamani wa Barca, Josep Maria Bartomeu na Sandro Rosell wote kwa pamoja wamehusishwa katika tuhuma hizo.
Bodi ya Real Madrid inadaiwa kufanya kikao jana Jumapili kujadiliana kuhusu sakata hilo na kutoa msimamo wao.
“Real Madrid inapenda kutoa dukuduku lake la ndani kuhusu suala hilo na inasisitiza imani yake katika mifumo ya sheria,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.
“Ili kulinda hadhi na haki zake, klabu itakuwa tayari kufika katika shauri hilo majaji watakapoanza kulisikiliza na kushirikisha pande zote zilizoathiriwa na tuhuma hizo,” ilifafanua klabu hiyo.
Rais wa Barcelona, Joan Laporta (pichani juu) amejibu hoja hizo akisisitiza kwamba klabu yake inafanywa mhanga wa kampeni hizo ili kuivunjia heshima na kuwataka mashabiki wao watulie.
“Hili halitushangazi na tutaitetea Barca na kuthibitisha kwamba klabu hii haijafanya kosa lolote,” alisisitiza Laporta.
Kimataifa Real Madrid yaigeuzia kibao Barca
Real Madrid yaigeuzia kibao Barca
Read also