Na mwandishi wetu
Yanga imeendelea kuimarisha nia yake ya kulitetea taji la Ligi Kuu NBC msimu wa 2022-23 baada ya leo Jumapili kuichapa Geita Gold mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa kwenye dimba la Azam Complex.
Ushindi huo mbali na kuiimarisha Yanga kileleni pia unazidi kuikatisha tamaa Simba inayoshika nafasi ya pili kwani sasa Yanga imefikisha pointi 65 hivyo kuizidi Simba kwa tofauti ya pointi nane. Timu zote hizo zimecheza mechi 24.
Jana Jumamosi Simba iliilaza Mtibwa mabao 3-0 na hivyo kujipa matumaini ya kuishusha Yanga kileleni kwa tofauti ya pointi tano lakini ushindi wa leo unamaanisha Simba imeongezewa mzigo wa pointi ili kuifikia Yanga.
Simba sasa inatakiwa iombee Yanga ipoteze mechi mbili ili kuishusha Yanga kileleni na hata kubeba ubingwa lakini nayo itatakiwa kushinda mechi zote ikiwamo mechi yao na Yanga.
Geita waliuanza mchezo wa leo kwa kasi wakionekana wenye kujiamini na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 18 baada ya Elius Maguli kuipatia timu hiyo bao kwa shuti la chinichini lililompita miguuni kipa wa Yanga, Diarra.
Pamoja na kuonekana kuzidiwa ujanja na Yanga, Geita hawakubabaika, walicheza soka la kawaida wakijihami na kufanya mashambulizi ya hapa na pale na kufanikiwa kulinda bao lao kwa kipindi chote cha kwanza.
Kipindi cha pili, Yanga ilikianza kwa kasi na dakika za 48 na 50 ilipata mabao mawili ya haraka haraka yaliyofungwa na Keneddy Musonda kwa kichwa na Clement Mzize kwa shuti hafifu la mguu wa kulia akimalizia mpira uliookolewa na kipa wa Geita, Yusuf Abdu.
Yanga waliendelea kufanya mashambulizi huku Geita wakijitahidi kutulia na kukabiliana na kasi ya mashambulizi hayo lakini walijikuta wakifungwa bao la tatu dakika ya 70 lililofungwa na Moloko.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, iliyochezwa leo, Coastal Union walishindwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani kuvuna pointi tatu baada ya kuambulia sare ya bao 1-1 kwa Singida Big Stars.
Matokeo hayo yanaifanya Coastal kufikisha pointi 26 na kujiimarisha katika nafasi ya 12 wakati Singida inapanda hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 48 na kuishusha Azam yenye pointi 47 hadi nafasi ya nne.
Soka Yanga yazidi kupaa kileleni
Yanga yazidi kupaa kileleni
Read also