Paris, Ufaransa
Lionel Messi amesema kwa sasa chaguo lake ni kuendelea kuichezea Paris St-Germain (PSG) lakini kwa sharti la kutaka ahakikishiwe kuwa timu hiyo itaendelea kuwa tishio katika kuwania mataji Ulaya.
Mkataba wa Messi na PSG unafikia ukomo majira ya kiangazi mwaka huu na zipo habari kuwa huenda akarudi timu yake ya zamani ya Barcelona ambayo mabosi wake wamenukuliwa wakisema wapo tayari kumpokea.
Habari ya Messi kuondoka PSG imepata nguvu baada ya timu hiyo juzi Jumatano kutolewa kwenye michuano mikubwa na yenye hadhi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya 16 bora.
Messi mwenye umri wa miaka 35 kwa sasa yupo kwenye mazungumzo na mabosi wa PSG wakiangalia uwezekano wa kuongeza mkataba wa mchezaji huyo na hivyo kuwa sababu ya kuibuka tena habari za mchezaji huyo kutaka kuihama PSG.
Messi ambaye pia amewahi kuhusishwa na mipango ya kurudi kwao Argentina kuichezea klabu yake ya utotoni ya Newell’s Old Boys, tangu atue PSG misimu miwili iliyopita ameifungia mabao 29 katika mechi 64.
Tamaa ya Messi kwa sasa ni kuona anabeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na PSG baada ya kufanya hivyo mara nne akiwa Barcelona na ndio maana ametoa sharti la kuhakikishiwa anabaki na timu yenye uwezo wa kupigania taji hilo kubwa barani Ulaya.
Habari za ndani zinadai kwamba Jorge Messi ambaye ni baba mzazi wa Messi na ndiye anayesimamia usajili wake, amekuwa na mazungumzo na mabosi wa PSG kuangalia namna ya kumbakisha mchezaji huyo katika klabu hiyo yenye makazi yake jiji la Paris.
Kimataifa Messi atoa masharti PSG
Messi atoa masharti PSG
Read also