London, England
Kocha wa Chelsea, Graham Potter ana kila sababu ya kuwa mwenye furaha baada ya timu yake kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo kuwa na amani baada ya kupitia kipindi kigumu.
Chelsea imekuwa na matokeo mabaya hasa katika Ligi Kuu England (EPL) licha ya usajili mkubwa ambao timu hiyo imeufanya lakini mambo yamekuwa magumu.
Ushindi wa jana Jumanne usiku wa mabao 2-0 dhidi ya Borrusia Dortmund umeibua matumaini mapya na kumpa amani Potter ambaye habari za kutimuliwa kwake zilikuwa zikivuma kwa kasi.
Baada ya matokeo hayo kocha huyo amenukuliwa akisema kwamba bado yupo, kauli ambayo inaweza kutafsiriwa kuwa ataendelea kuwa na timu hiyo baada ya matokeo hayo ya kuvutia.
Katika EPL, Chelsea sasa inashika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 34 imepoteza mechi tisa, nyingi kati ya hizo ni mechi za karibuni ambazo zilitishia nafasi ya Potter kiasi cha baadhi ya wachambuzi kuanza kuchambua majina ya makocha ambao wangeweza kuwa mbadala sahihi wa Potter.
Mabao ya Chelsea jana yalifungwa na Raheem Sterling dakika ya 43 na Havert kwa penalti dakika ya 53 na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kulala kwa bao 1-0 mechi ya kwanza.
Penalti hiyo ilizua utata baada ya picha za VAR kuonyesha kwamba Marius Wolf aliunawa mpira uliopigwa na Ben Chilwell lakini penalti ilipopigwa Havert kwanza alikosa lakini mwamuzi akaamuru irudiwe na ndipo Havert aliponi na kuujaza mpira wavuni.
“Wachezaji walikuwa vizuri na hata mashabiki walikuwa vizuri, tulikutana na timu inayofanya vizuri, katika mechi zilizopita niliona tulikuwa na kila sababu ya kusonga mbele, ni usiku wa kipekee,” alisema Potter baada ya mechi hiyo.
Pengine tangu aondoke Brighton na kutua Chelsea akichukua nafasi ya Thomas Tuchel, hii inakuwa mara ya kwanza kwa Potter kuwa mwenye furaha isiyo kifani baada ya kuwa na wakati mgumu.
Katika mechi nyingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Benfica ya Ureno iliibwaga Club Bruges mabao 5-1 na hivyo kufuzu robo fainali kwa jumla ya mabao 7-1.
Michuano hiyo itaendelea tena leo kwa mechi zifuatazo ambazo zitachezwa saa tano usiku…
Bayern Munich v PSG
Tottenham v AC Milan