Abidjan, Ivory Coast
Wakati Watanzania wakiomboleza msiba wa kifo cha beki wa Mtibwa Sugar, Iddy Mobby Mfaume, beki wa timu ya Racing Club d’Abidjan ya Ivory Coast, Moustapha Sylla naye amefariki dunia uwanjani wakati mechi ikiendelea.
Baada ya taarifa za kifo cha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, nyota wa zamani wa Chelsea na timu ya Taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba ametaka juhudi zaidi zifanyike kuwalinda wachezaji.
Sylla (pichani juu) alianguka na kufariki kwenye Uwanja wa Stade Robert Champroux katika mechi ya Ligi I iliyochezwa wikiendi hii kati ya Racing Club d’Abidjan iliyokuwa ikiumana na Sol FC d’Abodo.
Kabla ya kuanguka Sylla alikuwa kama mwenye kuhaha akitaka msaada kabla ya kuishiwa nguvu na kuanguka hali iliyowafanya wachezaji wa timu pinzani kumpa mwamuzi ishara ya kusimamisha mechi.
Baadaye mchezaji huyo alikimbizwa hospitali na maofisa wa huduma ya kwanza kabla ya taarifa za kifo chake kutangazwa wakati akipata matibabu hospitali ingawa haijaelezwa sababu ya kifo chake.
“Mchezaji alianguka wakati wa mechi ya Ligi I wakati akiiwakilisha timu yake ya Racing Club d’Abidjan iliyokuwa ikicheza na Sol FC d’Abodo,” alisema kiongozi mmoja wa soka Ivory Coast.
Akizungumzia kifo hicho, Drogba alituma salamu za rambirambi kwa wapenda soka wa Ivory Coast huku akikumbuka mwaka 2017 mchezaji mwenzake wa zamani wa kimataifa, Cheick Tiote alifariki uwanjani akiwa mazoezini.
Drogba ambaye ni balozi wa Fifa alisema kwamba hicho ni kifo cha mchezaji wa tatu wa Ivory Coast katika kipindi cha miaka minne na kutaka juhudi zifanywe kuwalinda wachezaji.
“Uko wapi utaratibu wa kila mchezaji profesheno kukutana na daktari? Vipi kuhusu vipimo vya damu, vipimo vya moyo, madawa ya wachezaji?” alihoji Drogba.
Taarifa ya klabu ya Racing Club d’Abidjan ilieleza kusikitishwa na msiba huo na kutuma salamu kwa ndugu wa familia ya marehemu na kumuombea apumzike kwa amani.
Sylla ambaye ni beki wa kushoto aliwahi kuichezea klabu ya Djoliba AC ya Mali na kushinda taji la ligi mwaka 2022 kabla ya kurudi nyumbani Ivory Coast Septemba mwaka jana na kujiunga na Racing Club d’Abidjan.

Kifo cha Sylla kimekuja wakati Watanzania bado wana kumbukumbu ya kifo cha beki wa Mtibwa, Mobby Mfaume aliyefariki mchana wa Jumapili baada ya kuugua ghafla wakati akifanya mazoezi binafsi kabla ya mechi ya Kombe la FA dhidi ya KMC, mechi ambayo Mtibwa ilishinda kwa bao 1-0.