Liverpool, England
Ushindi wa mabao 7-0 ambao Liverpool imeupata dhidi ya Man United umekuwa na maana kubwa zaidi kwa Mohamed Salah, umemfanya avunje rekodi katika historia ya klabu hiyo kwa kufikisha mabao 129.
Kwa idadi ya mabao hayo ya kwenye Ligi Kuu England, Salah amempiku mshambuliaji aliyekuwa akishikilia rekodi hiyo, Robbie Fowler ambaye kutokana na mafanikio yake mashabiki wa Liverpool walifikia hatua ya kumbatiza jina la ‘mungu’.
Mabao mawili aliyofunga katika ushindi huo uliopatikana Jumapili hii jioni, yanamfanya Salah ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Misri kuvunja rekodi ya Fowler akitumia mechi 205.
Katika mechi zote dhidi ya Man United, Salah pia anakuwa ameifunga timu hiyo mabao 10 hadi sasa na kumpiku nahodha wa zamani wa timu hiyo, Steven Gerrard ambaye ameifunga Man United mara nane.
Salah pia sasa anakuwa mchezaji anayeongoza kwa kuifunga Man United mabao mengi kuliko klabu nyingine yoyote ya Ligi Kuu England na hivyo anakuwa kama ndiye ‘adui mkubwa’ wa Man United.
Baada ya mafanikio hayo, Salah aliulizwa atafurahia wapi, naye akajibu kwa kifupi, “nikiwa nyumbani na familia yangu, tutakunywa chai na kulala.”
Katika mechi za mwanzo za msimu huu, Liverpool ilionekana kuyumba kidogo na kasi ya Salah katika upachikaji mabao haikuwa nzuri na hivyo kujengeka hoja kwamba kuondoka kwa Sadio Mane pia kumechangia hali hiyo.
Kwa ukubwa wa ushindi wa Jumapili dhidi ya Man United. timu ambayo imeanza kuwa tishio, si vibaya kuanza kuifikiria upya Liverpool na Salah kwamba huenda kasi ya timu hiyo ya msimu uliopita ndio imeanza kurudi.
Kimataifa Salah avunja rekodi ya mabao Liverpool
Salah avunja rekodi ya mabao Liverpool
Read also