London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amempongeza winga wake Reiss Nelson aliyefunga bao la dakika za nyongeza na kuipa timu hiyo ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Bournemouth, ushindi ambao Arteta anaamini unazidi kuwapa imani kwamba wanaweza kubeba taji la Ligi Kuu England.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii, Arsenal ikiwa nyumbani ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Philip Billing dakika ya kwanza tu ya mchezo na Marcos Senesi dakika ya 57.
Dakika tano baada ya Bournemouth kuandika bao la pili, Arsenal walipata bao la kwanza lililofungwa na Thomas Partey na kusawazisha dakika nane baadaye kwa bao lililofungwa na Ben White.
Wakati dakika zikiyoyoma, Nelson (pichani juu) aliihakikishia Arsenal pointi tatu muhimu katika dakika za nyongeza na kuamsha shangwe kwa mashabiki wake walioamini timu yao ingetoka uwanjani na pointi moja.
Baada ya bao hilo na filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa maofisa wa benchi la Arsenal walijazana uwanjani kwa furaha huku mashabiki wakiendelea kuwashuhudia majukwaani badala ya kuondoka.
Ushindi huo unazidi kufufua matumaini ya Arsenal kulibeba taji la EPL kwani timu hiyo imezidi kujiimarisha kileleni kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Man City inayoshika nafasi ya pili.
“Huenda hili ndio tukio kubwa na lenye kuvutia kwa wakati ambao tumekuwa pamoja,” alisema Arteta ambaye alijiunga na Arsenal Desemba 2019.
“Safari hii ambayo tumekuwa pamoja na namna mashabiki na wachezaji walivyoshikamana nayo, inalipamba tukio hili na kuwa la aina yake hasa,” aliongeza Arteta.
Tangu ipoteze mechi mbele ya Man City Februari 15, Arsenal imezifunga Aston Villa, Leicester City na sasa Bournemouth.
“Kushinda mechi nne katika ligi kuu ni jambo gumu na sisi tumeshinda mechi tatu kwa wiki jambo ambalo ni jambo gumu zaidi,” alisema Arteta.