Na mwandishi wetu
Hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) inatarajiwa kumalizika leo Jumapili kwa mechi mbili zinazotarajiwa kuchezwa kwenye viwanja viwili vya miji tofauti.
Kagera Sugar ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba itawaalika Mbeya City na Azam FC itakuwa mwenyeji wa Mapinduzi ya Mwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Washindi wa mechi hizo wataungana na timu za Simba, Yanga, Singida Big Stars, Ihefu, Geita Gold na Mtibwa Sugar kwenye hatua ya robo fainali.
Kocha Mkuu wa Kagera, Mecky Maxime alisema wamejiandaa vema na mchezo huo kwani ni muhimu kwao kufuzu robo fainali na wataingia kwa tahadhari kwa sababu Mbeya City si timu ya kubeza.
“Tumejiandaa vema na mchezo na wachezaji wana morali na tutaingia kwa tahadhari uwanjani kwa sababu Mbeya City ina wachezaji bora kama ilivyo kwa kikosi chetu,” alisema Maxime.
Aidha, Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Noliega Mwamlima alisema wamejiandaa vya kutosha kwa mchezo huo na tayari wamewasili na kikosi chake Bukoba mapema tayari kwa mchezo huo.
“Tunajua tunacheza na mwenyeji ambaye anajua kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani ila na sisi tumejiandaa vema kuhakikisha tunapata ushindi na kufuzu robo fainali msimu huu,” alisema Mwamlima.
Kwa upande wa kocha msaidizi Azam, Kali Ongala alisema wamejiandaa dhidi ya wapinzani wao kwa kuupa uzito mchezo huo kwa namna unavyostahili licha ya kuwa wanacheza na timu ya daraja la chini.
“Mapinduzi ni mabingwa wa mkoa wa Mwanza na sisi tunajua timu za madaraja ya chini zinajua kung’ang’ania timu kubwa, tumejiandaa kuhakikisha tunashinda, mchezo huu muhimu kwetu,” alisema.
Martin Mahimbo ambaye ni kocha mkuu wa Mapinduzi alisema wamekuja Dar es Salaam kwa kazi moja ya kutafuta ushindi kwani kikosi chake kimeiva na kipo kamili kuivaa Azam FC.
“Tumefika hapa, hatua hii kutokana na kiwango chetu kuwa bora na kesho (leo) tunaenda kuwaonesha Azam kandanda halisi linavyosakatwa, hivyo tunawaomba Wanamwanza waishio Dar es Salaam waje kwa wingi kuwashangilia vijana wao,” alisema.