Na mwandishi wetu
Nyota ya beki wa kati wa Simba, Henock Inonga imezidi kung’ara, kwa takriban siku 10 zilizopita mchezaji huyo amejikuta katika matukio makubwa manne ya kujivunia.
Ameifungia Simba bao pekee na la kwanza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, yumo kwenye timu ya wiki ya ligi hiyo, ameitwa timu ya Taifa ya DR Congo na leo Alhamisi ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mashabiki wa mwezi Februari.
Katika kinyang’anyiro cha mchezaji bora wa mwezi wa Simba, Inonga alikuwa akichuana na beki mwenzake, Shomari Kapombe na kiungo wa kati, Mzamiru Yassin ambao aliingia nao tatu bora.
Inonga ambaye ni raia wa DR Congo ametangazwa leo kushinda tuzo hiyo ambayo mshindi hupatikana kwa kupigiwa kura na mashabiki.
Mtandao wa Klabu ya Simba, umetoa mchanganuo wa kura za kinyang’anyiro hicho ambapo Inonga ameibuka kidedea kwa kura 498, Kapombe akipata 246 na Mzamiru 115. Mzamiru alishinda tuzo hiyo mwezi Novemba, mwaka jana.
Inonga ambaye kwa ushindi huo, atakabidhiwa Sh 2,000,000 na tuzo kutoka kwa wadhamini wa tuzo hiyo, Emirate Aluminium Profile, sasa anashinda kwa mara ya pili tuzo hiyo ambapo aliinyakua pia msimu uliopita mwezi Aprili akiwashinda Joash Onyango na Kapombe.
Mashabiki wa Simba bado wanamkumbuka Inonga kwa kufunga bao pekee na la ushindi katika mchezo wao uliopita wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers na hivyo kuitoa timu hiyo kimasomaso ugenini.
Inonga pia ndiye mchezaji pekee wa Simba pamoja na Fiston Mayele wa Yanga kati ya wachezaji wote wa DR Congo wanaocheza soka nchini ambao wameitwa timu ya Taifa ya nchi hiyo na kocha Sebastien Desabre.
DR Congo inajiandaa kuumana na Mauritania katika mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023)
Soka Nyota ya Inonga yazidi kung’ara
Nyota ya Inonga yazidi kung’ara
Read also