Seul, Korea Kusini
Nahodha na beki wa Man United, Harry Maguire amesema kwamba anaungwa mkono na kocha wake, Erik ten Hag lakini amekiri kuchoka kukaa benchi na anataka apewe nafasi ya kucheza.
Tangu kuanza msimu huu, Maguire ameanza mechi tisa tu na aliingia dakika mbili za mwisho katika mechi ya fainali ya Carabao Jumapili iliyopita, mechi ambayo United iliichapa Newcastle mabao 2-0 na kubeba taji hilo.
Katika beki ya kati Man United, Ten Hag anapenda kuwatumia, Raphael Varane na Lisandro Martinez na Maguire anakiri kiwango bora cha wachezaji hao kimemfanya awe na wakati mgumu kupenya kikosi cha kwanza.
“Mimi ni mchezaji ambaye nataka kucheza mechi tangu mwanzo, kuwaongoza vijana kutokea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo lakini pia naelewa hii ni sehemu ya soka, unapocheza katika soka la hadhi ya juu kunakuwa na ushindani mkubwa wa nafasi,” alisema Maguire.
“Jamaa wanaoanza, Rapha anacheza vizuri mno na tunaona mawazo yake, ni vile anavyotaka kocha, anacheza beki wa kati, anatumia mguu wa kushoto, kwa hiyo ushindani ni mkubwa,” alisema Maguire.
Ten Hag tangu atue Man United ameendelea kumuamini Maguire katika nafasi ya unahodha licha ya ya mchezaji huyo kutokuwa na uhakika wa moja kwa moja wa kupata nafasi kikosi cha kwanza tangu Agosti mwaka jana.
Kinachoonekana sasa ni kwamba mchezaji huyo anataka kuhama na huenda dirisha la usajili majira ya kiangazi akaondoka ingawa katika dirisha dogo la Januari alidaiwa kukataa ofa ya kusajiliwa West Hem.
“Nafikiri kocha (Ten Hag) amekuwa akiulizwa mara kadhaa kuhusu mimi na majukumu yangu na amekuwa wazi kuwa ananiamini lakini hili ni soka na hii ni Manchester United, tunataka kushinda mataji, mataji makubwa na ili kufanya hivyo unahitaji ushindani wa kuwania namba,” alisema Maguire.