Manchester, England
Kocha wa Man United, Eric ten Hag amempongeza mchezaji wake Fred kwa namna alivyompunguza makali kiungo wa Barca, Frankie de Jong kwa kumsumbua kama mbu.
Katika mechi hiyo ya Europa Ligi iliyochezwa Alhamisi usiku, Man United ilitoka na ushindi wa mabao 2-1 na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3 baada ya sare ya mabao 2-2 katika mechi ya awali.
Fred (ichani ndiye aliyefunga bao la kusawazisha la Man United muda mfupi baada ya mapumziko na kutoa mchango mkubwa katika bao la pili na la ushindi la timu hiyo lililofungwa na Mbrazil mwenzake Antony.
Katika mechi hiyo Fred alipewa kazi maalum ya kumkata makali kiungo huyo wa Barca, De Jong, kazi ambayo aliifanya vizuri hadi kupongezwa na Ten Hag.
“Tayari alishakuwa na jukumu muhimu wiki iliyopita tukiwa Barcelona na wiki hii ni hivyo hivyo, kwanza kazi yake kubwa ilikuwa ni kumzuia Frenkie asicheze,” alisema Ten Hag.
“Alilazimika kucheza kwa kumzunguka mithili ya mbu na kuwa nyuma yake wakati wote, aliifanya kazi hiyo kwa namna nzuri, wiki iliyopita alitoa pasi kwa Rashford aliyefunga goli na safari hii amefunga goli, kiwango kizuri,” alisema Ten Hag.
Wakati huo huo, kocha wa Barca, Xavi Hernandez baada ya timu yake kutolewa katika Europa Ligi, amesema sasa wanachofanya ni kujipanga kwa ajili ya msimu ujao kwenye michuano ya Ulaya.