Manchester, England
Man United leo Alhamisi inaumana na Barca katika mechi ya Europa Ligi, mechi ambayo kocha wa timu hiyo, Eric ten Hag amesema ili washinde ni lazima wacheze katika kiwango bora cha msimu huu.
Katika mechi iliyopita ambayo Man United walikuwa ugenini timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na leo Man United watakuwa nyumbani Old Trafford.
“Unapokutana na timu kubwa kama hizo unalazimika kucheza katika ubora wako vinginevyo huna nafasi,” alisema Ten Hag.
Baada ya mechi ya leo ambayo ni ya hatua ya 16 bora, Jumapili Man United wana mechi nyingine ya fainali ya kukata na shoka dhidi ya Newcastle kuwania taji la Carabao kwenye dimba la Wembley.
Wakifanikiwa kulibeba taji hilo, itakuwa mara ya kwanza kwa kocha Ten Hag kubeba taji akiwa na timu hiyo lakini pia litakuwa taji la kwanza kwa timu hiyo tangu mwaka 2017.
Kama hiyo haitoshi Machi Mosi, timu hiyo itakuwa na mechi ya Kombe la FA raundi ya tano dhidi ya West Ham, mechi ambayo wakishinda pia watakuwa wamepiga hatua muhimu katika mbio za kusaka taji hilo.
Katika Ligi Kuu England (EPL) pia huwezi kuitoa Man United katika mbio za kuliwania taji hilo msimu huu, inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49, imezidiwa na vinara Arsenal kwa pointi tano na pointi tatu dhidi ya Man City inayoshika nafasi ya pili.
“Tuna fursa lakini fikra za kwanza wakati wote ni katika mechi inayofuata, na hatuwezi kubeba taji la Europa Ligi wiki hii, ni lazima tujiweke katika mtazamo kwamba kila siku tunatakiwa kuwa na malengo yaliyo bora kwa ajili yetu,” alisema Ten Hag.
Ten Hag pia alizungumzia kitendo cha yeye kupata chakula cha jioni na kocha wa zamani wa Man United, Sir Alex Ferguson aliyeweka rekodi ya kubeba mataji 13 akisema kwamba jambo hilo lilikuwa na maana kubwa kwake.
“Wakati wote nafurahia kuzungumza na watu ambao wana uelewa wa mambo, uzoefu mkubwa, anataka kushirikisha watu, anataka kukusaidia na kukuunga mkono,” alisema Ten Hag.
“Unaona kama vile Manchester United ni klabu yake, anaona anatakiwa kujitoa kwa klabu na anataka kuona tunafanya vizuri, ulikuwa usiku mzuri na nafikiria siku nyingine ya kukutana naye kwa chakula cha jioni,” alisema.
Winga wa Man United, Antony na beki Harry Maguire wako fiti kwa mechi hiyo baada ya kuwa majeruhi wakati mshambuliaji Anthony Martial bado majeruhi na beki Lisandro Martinez na kiungo Marcel Sabitzer wamemaliza adhabu.
Barca leo itawakosa viungo Pedri ambaye ni majeruhi na Gavi anayetumikia adhabu huku mshambuliaji Mfaransa Ousmane Dembele hatokuwapo kwa kuwa bado anasumbuliwa na misuli ingawa kiungo mkongwe, Sergio Busquets aliyekuwa na matatizo ya enka kwa sasa yuko fiti.
Kocha wa Barca Xavi akiizungumzia mechi hiyo alisema: “Hakika itakuwa mechi ngumu, Manchester United ni moja ya timu bora za Ulaya na hilo wamekuwa wakilithibitisha.
Mechi za Europa Ligi leo Alhamisi ni kama ifutavyo…
Man Utd v Barcelona
FC Midtjylland v Sporting
Monaco v B Leverkusen
Nantes v Juventus
PSV Eindhoven v Sevilla
Union Berlin v Ajax
Rennes v Shakhtar Donetsk
Roma v RB Salzburg