Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imetoa taarifa kukanusha habari zinazoendelea kusambaa kuwa wameachana na kocha wao mkuu, Robert Oliveira ‘Robertinho’ badala yake wamesisitiza kuwa kocha huyo bado yupo Simba.
Simba wameeleza hayo leo Jumatano wakifafanua kwamba kumekuwa na taarifa za kupotosha kwenye vyanzo mbalimbali hasa mitandao ya kijamii kuhusu wao kuachana na kocha huyo raia wa Brazil.
Kupitia ukurasa wao wa Instagram, Simba wameandika: “Taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu mkataba wa Kocha Robertinho si sahihi. Anaendelea na majukumu yake ya kuandaa kikosi kuelekea mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika.”
Fununu za timu hiyo kutaka kumtimua kocha huyo aliyetua takriban miezi miwili iliyopita zimeibuka baada ya matokeo mabaya ya mechi tatu za Simba zilizopita.
Wiki iliyopita, Simba ilipoteza michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya ya Guinea kwa kufungwa bao 1-0 na Jumamosi iliyopita ililala kwa mabao 3-0 mbele ya Raja Casablanca ya Morocco na jana Jumanne ilitoka sare ya bao 1-1 na Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu NBC.
Matokeo hayo yameifanya Simba kuwa na wakati mgumu kwenye mechi nne zilizobaki za makundi kuwania kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, pia kuzidi kufifisha mbio zao za kulibeba taji la Ligi Kuu NBC.
Simba inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu NBC ikiwa na pointi 54 nyuma ya kinara Yanga yenye pointi 59 ambayo leo jioni wataumana na KMC.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu ameiambia GreenSports kuwa matokeo hayo hayamaanishi kuwa hawamo kwenye kupambana kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Badala yake Mangungu amefafanua kwamba wanaendelea kujipanga zaidi ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye michezo iliyobaki.
Simba watashuka dimbani Februari 25, mwaka huu kuumana na Vipers SC ya Uganda katika mchezo wa tatu wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Uwanja wa St. Mary’s, Entebbe, Uganda.
Soka Robertinho bado yupo sana Simba
Robertinho bado yupo sana Simba
Read also