Barcelona, Hispania
Mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil na klabu ya Barcelona, Dani Alves ataendelea kusota rumande baada ya jaji kumnyima dhamana katika kesi ya udhalilishaji kijinsia inayomkabili.
Alves kwa mara ya kwanza alikamatwa kwa tuhuma hizo mapema Januari mwaka huu na Januari 20 mawakili wake waliwasilisha rufaa wakiomba apewa dhamana lakini jana Jumanne rufaa ilikataliwa.
Akipinga kutoa dhamana, jaji katika mahakama hiyo ya mjini Barcelona, alisema kwamba Alves ni mtu mwenye uwezo wa kifedha na anaweza kuondoka wakati wowote hasa kwa kuwa ni raia wa Brazil nchi ambayo Hispania haina mamlaka nayo ya moja kwa moja.
Alves mwenye umri wa miaka 39 anatuhumiwa kwa kumdhalilisha mwanamke katika klabu moja ya usiku mjini Barcelona, tukio ambalo anadaiwa kulifanya Desemba 30 mwaka jana.
Uchunguzi wa awali wa tuhuma hizo ulianza kufanywa mapema Januari lakini mchezaji huyo alikamatwa Januari 20 baada ya kupokea taarifa yake na ya msichana anayedaiwa kudhalilishwa.
Akitoa sababu za kumnyima Alves dhamana jaji huyo alisema kwamba uamuzi wake ulizingatia matokeo ya uchunguzi wa kisayansi yaliyofanyika kwa msichana anayedaiwa kufanyiwa udhalilihaji huo, kamera pamoja na taarifa aliyoitaja kuwa yenye kujichanganya iliyotolewa na Alves.
Alves ambaye amekana tuhuma hizo alilazimika kusafiri kutoka Mexico anakocheza soka katika klabu ya Pumas hadi Hispania kwa ajili ya kesi hiyo ingawa klabu ya Pumas tayari imevunja mkataba naye.
Mchezaji huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha Barcelona kilichoitwa kikosi cha dhahabu ambacho kilitamba barani Ulaya kwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulata mara tatu kikiwa na kina Lionel Messi, Xavi, Iniesta, Puyol na wengineo.
Mbali na Barcelona na timu ya Taifa ya Brazil, Alves pia barani Ulaya pekee amewahi kuzichezea kwa mafanikio klabu za Sevilla ya Hispania, Juventus ya Italia na PSG ya Ufaransa.
Kimataifa Alves anyimwa dhamana
Alves anyimwa dhamana
Read also