Na Hassan Kingu
Simba hii tusiidharau, bado ina nafasi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kufungwa mabao 3-0 na Raja Casablanca ya Morocco na hivyo kupoteza mchezo wa pili baada ya kufungwa bao 1-0 na Horoya FC ya Guinea.
Kipigo cha mabao 3-0 na ushindi wa Yanga wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, Simba wanajiona kama wamepigwa mara mbili, Jumamosi walifungwa wao na Jumapili wakafungwa midomo.
Maana yake ni kwamba ushindi wa Yanga ni kama vile umewafunga midomo Simba kwamba wanabezwa na Yanga na hawana la kusema.
Ukiweka kando ushabiki, Simba hawana sababu ya kuwa wanyonge baada ya kupoteza mechi mbili na waache kujilinganisha na Yanga kwani kwa sasa wanacheza michuano miwili tofauti, Simba wanacheza Ligi ya Mabingwa na Yanga wanacheza Kombe la Shirikisho.
Japo wote wanacheza soka kwa kanuni na sheria zile zile lakini sehemu kubwa ya timu shiriki za Kombe la Shirikisho ni zile zilizokwama ama katika ligi ya ndani kwa kushindwa kubeba taji au kwenye Ligi ya Mabingwa na kuangukia Kombe la Shirikisho.
Kwa maana nyingine Ligi ya Mabingwa inashirikisha timu zilizo bora zaidi kuliko zile za kwenye Kombe la Shirikisho, huo ndio ukweli usio na chembe ya shaka. Kwa maana nyingine Simba wanashiriki michuano mikubwa na migumu kuliko Yanga.
Unapoizungumzia Raja Casablanca ya sasa huwezi kuilinganisha na Mazembe ya sasa, zote ni timu za soka lakini Raja ipo juu na haishangazi inapoifunga Simba 3-0 au inapoifunga Vipers mabao matano.
Kwa nini Simba ina nafasi?
Kigezo cha kwanza kabisa cha imani yangu ni kwenye mechi na Raja, japo Simba ilifungwa lakini ilionyesha uhai na kama ingetumia vizuri nafasi ilizotengeneza basi huenda ingebadili matokeo.
Tumeona Pape Sakho, John Bocco na Jean Baleke walivyopata nafasi lakini wakashindwa kuzitumia kuipa Simba ushindi, nafasi hizo tatu moja tu ingetumiwa vizuri ingekuwa faida kubwa kwa Simba.
Raja walipata bao la kwanza dakika ya 30, dakika tano baadaye Sakho akashindwa kuitumia vizuri pasi ya Saido Ntibazonkiza kuipa Simba bao.
Kwa ujumla katika dakika 20 tangu kuanza kipindi cha pili, Simba ilionyesha uhai ikitengeneza nafasi na kufika langoni mwa Raja mara kwa mara huku Raja wakitumia muda mwingi kuzuia na kutibua mipango ya Simba.
Matumaini ya wachezaji wa Simba kupata bao la kusawazisha yalikuwa wazi na yalijidhihirisha katika uchezaji wao kwa namna walivyokuwa wakipambana na kuonyesha dalili zote kwamba walikuwa na uwezo wa kupata bao la kusawazisha.
Mfano muangalie Shomari Kapombe katika muda huo ungeweza kudhani kwamba alikuwa mshambuliaji kwa namna ambavyo alikuwa huru kupanda hadi akajikuta akichezewa rafu kwa bahati mbaya na Ntibazonkiza wakiwa katika eneo la Raja.
Katika dakika ya 70 mmoja wa mashabiki niliyekuwa karibu naye nilimsikia akisema kwamba Simba wanafanya kazi kubwa ya kutafuta bao lakini hawajalipata, hofu yake ni kwamba Raja wakitumia nafasi chache walizotengeneza kupata bao litaivuruga Simba.
Dakika kama 15 baada ya kauli hiyo, Raja wakapata bao la pili, shabiki yule yule akasema bao hilo litawavuruga wachezaji wa Simba kisaikolojia kwa kuwa juhudi kubwa walizozifanya zimeshindwa kuzaa matunda, watachanganyikiwa wasijue watafute bao la kufutia machozi au wazuie la tatu.
Kwa kauli hiyo sikushangazwa na bao la tatu la Raja ambao walionyesha ubora wao, hadhi yao na uwezo wao wa kubadili mchezo katika mazingira magumu kwani kwa namna walivyoshambuliwa na Simba ingetarajiwa watumie muda mwingi kupaki basi na si kutafuta bao.
Mazingira ya mechi ya Raja na uwezo uliooneshwa na wachezaji wa Simba hasa katika kutafuta bao la kusawazisha yananifanya niamini kwamba Simba inaweza kumaliza katika nafasi nzuri kwenye kundi lake na kusonga mbele.
Simba iliyokuwa nyumbani na kuonyesha uwezo wa kutafuta bao katika mechi na Raja ina uwezo wa kufanya hivyo katika mechi za nyumbani na hata ugenini dhidi ya Horoya na Vipers.
Mechi ngumu dhidi ya Raja inatosha kuwa sababu ya kutambua ugumu wa Ligi ya Mabingwa lakini inatosha pia kuwa somo la kujua ni vipi Simba itacheza mechi nne zilizobaki, ugenini dhidi ya Raja na nyumbani na ugenini dhidi ya Vipers na nyumbani dhidi ya Horoya.
Ushindi katika mechi hizo unawezekana, Ligi ya Mabingwa ni michuano migumu, Vipers alipofungwa mabao matano na Raja kuna mashabiki walianza kuitaja timu hiyo kuwa ni kibonde katika kundi la Simba, si kweli Vipers ni vibonde wa Raja na si timu zote za Kundi C.
Raja ndio vinara wa Kundi C wakiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zote mbili wakifuatiwa na Horoya wenye pointi 4, Vipers yenye pointi moja ni ya tatu na Simba inashika mkia ikiwa haina pointi.
Soka Simba hii tusiidharau, ina nafasi
Simba hii tusiidharau, ina nafasi
Read also