Barcelona, Hispania
Leo Alhamisi, Man United na Barca zinaumana katika Europa Ligi huku kocha wa Barca, Xavi Hernandez (pichani) akimtaja, Marcus Rashford wa Man United kuwa ni kati ya washambuliaji tishio duniani.
Xavi ambaye timu yake itakuwa mwenyeji wa mchezo huo, pia alimpongeza kocha wa Man United, Eric ten Hag kwa namna alivyoibadili timu hiyo na kuifanya iwe tishio.
“Ten Hag ni kocha mzuri, kwa mtazamo wangu naamini kwa kiasi fulani amebadili mambo United, si kazi rahisi lakini ameifanikisha, wanavutia kwa mara nyingine, kuanzia klabu, mashabki na hata aina ya uchezaji wao,” alisema Xavi.
“Anabadili mambo kuanzia kuwa tishio kwa timu pinzani, kujilinda yaani kila mmoja anafanya kazi vizuri, kwa hiyo ni mpinzani mgumu kwetu na yeye (Ten Hag) ni kocha safi,” alisema.
Rashford kwa upande wake ameendelea kuwa vizuri chini ya kocha huyo Mholanzi akiwa tayari amefunga mabao 13 katika mechi 15 baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia.
Xavi alisema kwamba wana wajibu wa kujilinda dhidi ya wachezaji wote wa Man United lakini zaidi ni Rashford ambaye alisema kwamba kwa sasa ni mchezaji tishio zaidi Ulaya.
Kwa upande wake Ten Hag naye alimpongeza Xavi akisema kwamba kiungo huyo wa zamani wa Barca anaipeleka timu hiyo katika mwelekeo sahihi baada ya kuwapo hitaji kubwa la kufanya mabadiliko kwenye timu hiyo.
Ratiba ya mechi za Europa Ligi leo Alhamisi…
Barcelona vs Man Utd
Ajax vs Union Berlin
RB Salzburg vs Roma
Shakhtar Donetsk vs Rennes
B Leverkusen vs Monaco
Juventus vs Nantes
Sevilla vs PSV Eindhoven
Sporting vs FC Midtjylland